Bei za mafuta ya Taa, Petroli, Dizeli Yashuka Dar

Bei za mafuta ya Taa,  Petroli, Dizeli Yashuka Dar
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kushuka kwa bei za rejareja za Petroli, Dizeli na mafuta ya Taa kwa asilimia 0.43 (shilingi 10) na asilimia 0.83 (shilingi 19) na asilimia 1.05 (shilingi 24 kwa lita).


Huku bei za jumla za Petroli ikiwa imepungua kwa shilingi 10 kwa lita sawa na asilimia 0.45, Dizeli shilingi 18.95/lita sawa na asilimia 0.87 huku bei ya mafuta ya Taa ikipungua kwa asilimia 1.11 sawa na shilingi 23.78/lita.

Kwa mwezi Septemba 2018, bei za rejareja za Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini zimeongezeka kwa shilingi 114/lita (sawa na asilimia 5.11) na shilingi 102/lita (sawa na asilimia 4.70).

Bei za jumla za Petroli na Dizeli zikiongezeka kwa shilingi 113.70/lita (sawa na asilimia 5.39) na shilingi 101.50/lita (sawa na asilimia 4.97), ambapo ongezeko hilo kwa mkoa wa Tanga limetokana na ongezeko la bei za mafuta hayo katika soko la dunia kwa mwezi Julai 2018 ikilinganishwa na zile za mwezi Machi 2018, zilizokuwa zikitumika tangu shehena ya mwisho kupokelewa katika bandari ya Tanga.

Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Nzinyangwa Mchany na kusisitiza kuwa bei hizo zitaanza kutumika rasmi leo Septemba 05, 2018 huku akiwataka wauzaji mafuta kufuata sheria na kanuni husia.

"Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani", amesema Nzinyangwa.

Pamoja na hayo, taarifa hiyo imeendelea kwa kusema "ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika".

Mbali na hilo, EWURA imewataka wauzaji wa mafuta ya petroli kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) huku wanunuzi wakiombwa kuhakisha wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

"Stakabadhi hizo za malipo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya aidha kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa", amesisitiza Nzinyangwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad