Billnass amebainisha hayo alipokuwa anazungumza kwenye Backstage ya Bongo Fleva TOP20 inayorushwa na East Africa Radio, baada ya kuwepo dhana kutoka kwa wasanii wengi kutegemea kufanya 'collabo' nyingi kuliko kutengeneza kazi ya pekee yake, kwa kile wanachokidai wanajitangaza katika game ya muziki bila ya kufikilia upande wao pili.
"Kama kweli msanii anataka kutengeneza faida kubwa katika kazi zako na kuwepo kwa muda mrefu kwenye 'game', mara nyingine unapaswa usimame mwenyewe ili uweze kujipa uzoefu kwa kile unachokifanya, maana muda mwingine unaweza kujikuta unashindwa kupiga 'show' vizuri kwasababu watu wanamtaka msanii fulani uliyemshirikisha katika kazi yako", amesema Billnass.
Mbali na hilo, Billnass amekiri kuwa katika wasanii walioweza kufanikiwa kupitia njia hiyo ni Mr. Nice, kutokana kazi zake nyingi alifanya peke yake.
"Mimi naamini katika watu waliowahi kufanikiwa zaidi kwenye muziki ni Mr. Nice kwasababu karibu albamu yake nzima hakuwa na 'collaboration', 'so' nasi wasanii wa sasa tunatakiwa tufanye hivyo", amesisitiza Billnass.
Billnass ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wasanii wa hiphop, wakiwatuhumu waimbaji wa bongo fleva kuwanyima 'collabo' kwa kuhofia kuharibiwa kazi zao licha ya kuwa hao wa bongo fleva kupewa collabo kila uchao na wana hiphop.