Akiongea na wananchi katika eneo hilo la Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara, Rais alimruhusu binti aitwaye Monica Bernad mwanafunzi wa kidato cha tano, katika shule ya Ingwe kueleza kero zilizopo katika shule hiyo ya Upili, ambapo alitaja kero kadhaa kama upungufu wa mabweni na madarasa.
''Kwanza Monica nikushukuru sana lakini si ajabu vijana wa kiume wa Nyamongo wameshaanza kumwangalia angalia na pengine kufikiria kumtorosha, washindwe kabisa wasimsogelee Monica ambaye ameongea kwa niaba ya wanafunzi na vijana wengi'', alisema Magufuli.
Mwanafunzi Monica Bernad kushoto na Rais Magufuli kulia kwenye mkutano leo Nyamongo
Aidha katika kutatua kero za shule hiyo Rais aliendesha harambee ndogo katika mkutano huo wa hadhara ambapo viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani, Wabunge na Mawaziri walichangia na kuwezesha kupatikana kwa takribani shilingi milioni 24.
Mwisho Rais Magufuli yeye alichangia kiasi cha shilingi milioni 5, hivyo kufikisha zaidi ya milioni 29 ambazo amewaagiza Mkuu wa mkoa na RPC kuhakikisha zinakusanywa na kwenda kutumika kama ilivyokusudiwa ili wanafunzi katika shule ya Ingwe wasome bila shida.