Binti amfanya Rais Magufuli achangishe fedha Baada ya Kumtajia Matatizo ya Shule yao


Akiwa katika mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo kwasasa yupo Mkoani Mara Rais Magufuli, leo ameendesha harambee ndogo katika eneo la Nyamongo ya kuchangia fedha kwa ajili ya kutatua kero katika shule ya Ingwe, huku akiwataka wanaume katika eneo hilo kuacha mawazo


Akiongea na wananchi katika eneo hilo la Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara, Rais alimruhusu binti aitwaye Monica Bernad mwanafunzi wa kidato cha tano, katika shule ya Ingwe kueleza kero zilizopo katika shule hiyo. 

Alipokabidhiwa kipaza sauti, Monica alianza kwa kusema kuwa shule hiyo inakumbana na changamoto nyingi ikiwamo upungufu wa walimu pamoja na vitabu.

“Shule yetu imeanza mwezi wa saba tarehe 30 kama High School lakini shule yetu ina upungufu wa walimu na vitabu kwa o-level na advanced level,” alisema mwanafunzi huyo.

Pia alieleza kuwa wana uhaba wa mabweni, hali inayosababisha wanafunzi kuchangia vitanda.

“Tuna bweni moja ambalo ‘tunashea’ wanafunzi wa o-level na advanced wa kike, katika bweni hilo tuna vitanda vichache ambapo inasababisha kitanda cha futi mbili na nusu tunalala wanafunzi watatu,” amesema.

Pia ametaja mambo mengine kuwa ni upungufu wa vyumba vya madarasa, viti, maji, umeme na ukosefu wa gari la wagonjwa.

“Tunakosa vitabu rejea kwa kidato cha tano na cha sita na inatufanya kutumia kitabu kimoja kwa kuchangia na vitabu hivi shuleni havipo. Mheshimiwa Rais tunatoka katika familia maskini tunaomba ututatulie tatizo hili,” amesema.

Baada ya kusikiliza kero hizo, Rais Magufuli alisema;


''Kwanza Monica nikushukuru sana lakini si ajabu vijana wa kiume wa Nyamongo wameshaanza kumwangalia angalia na pengine kufikiria kumtorosha, washindwe kabisa wasimsogelee Monica ambaye ameongea kwa niaba ya wanafunzi na vijana wengi'', alisema Magufuli.


Aidha katika kutatua kero za shule hiyo Rais aliendesha harambee ndogo katika mkutano huo wa hadhara ambapo viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani, Wabunge na Mawaziri walichangia na kuwezesha kupatikana kwa takribani shilingi milioni 24.


Mwisho Rais Magufuli yeye alichangia kiasi cha shilingi milioni 5, hivyo kufikisha zaidi ya milioni 29 ambazo amewaagiza Mkuu wa mkoa na RPC kuhakikisha zinakusanywa na kwenda kutumika kama ilivyokusudiwa ili wanafunzi katika shule ya Ingwe wasome bila shida.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad