Mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa Robert Kyagulanyi amemshutumu Rais Museveni kwa madai kwamba anawahonga vijana nchini Uganda kwa sababu ya kile alichodai ni mwenendo wake kujitenga kutoka kwa watu wa kawaida.
"Rais wetu amejitenga sana na vijana kiasi kwamba wanaamini hakuna mtu anayeweza kusema nao chochote bila kuwapa rushwa. Hiyo ndiyo sababu wanakwenda wakijaribu kuwapa rushwa vijana hawa," alisema Kyagulanyi katika mahojiano maalum Jumatatu jioni na redio 933 KFM.
Mbunge huyo maarufu kwa jina la Bobi Wine alisema saa kadhaa baada ya Rais Museveni kutoa Sh100 milioni kwa vijana wa kitongoji cha Kamwokya nje kidogo ya Kampala, kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Kanali Shaban Bantariza, naibu mkurugenzi wa Kituo cha Afya Uganda, aliyemwakilisha Rais katika kanisa la Mavuno ya Pasaka (Passover Harvest Church) ambako vijana walipewa fedha aliwataka wanufaika wa msaada huo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyowekwa.
"Rais amewapa ninyi fedha hizi, lakini nawahimiza kutumia vizuri kwa sababu mmepewa Sh 100 milioni na kama mtatumia vizuri, katika siku zijazo mtapata zaidi ya hizi," alisema Kanali Bantariza.
Alisema pia kwamba fedha hizo zitatumika katika vikundi vya vijana vilivyosajiliwa kama Saccos.
Septemba 14, Rais Museveni pia alizindua zaidi ya miradi 10 aliyoipa fedha kupitia saccos katika wilaya za Kampala na Wakiso.
Hata hivyo, Bobi Wine alisisitiza: “Fedha ambazo Museveni anatumia kuhonga vijana na watu wa kawaida ni kwa ajili ya ukombozi wao (kina Museveni).
Alisema utawala umejawa hofu kuona watu wanaunganika kwa sababu ya hoja moja ya msingi na ndiyo maana wanasambaza askari wenye silaha nzito kuzunguka Kampala siku aliporejea kutoka Marekani wiki iliyopita.
“Utawala unataka watu waendelee kuwa watumwa na waoga...Wanahofia watu kuungana pamoja. Hawajawahi kuona watu wakizungumza sauti moja. Lakini wakati utafika hata kama nitakuwa kwenye nyumba yangu, watu wataendelea kupigania haki zao kwa sababu nimeeleza wazi hii si kwa ajili ya Bobi Wine; ni kuhusu mamlaka ya watu. Nafurahi kwamba watu wanafunguka macho kwa kasi,” alisema.