Hatimaye msanii mkubwa nchini Uganda ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kyadondo, Bobi Wine amefunguka kwa mara ya kwanza tangu alivyopatwa na majanga ya kukamatwa na wanajeshi hadi kufunguliwa mashtaka.
Bobi Wine ambaye yupo nchini Marekani akipatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata kwenye sakata hilo, amesema kuwa usiku wa Agosti 13, 2018 akiwa katika hoteli moja mjini Arua alisikia wanawake nje ya hoteli wakipigwa na wanaume waliokuwa wanawauliza Bobi Wine yupo chumba namba ngapi.?
Bobi ameeleza kuwa wanawake hao ambao walikuwa ni wahudumu wa Hoteli hiyo, walikataa katu katu kutaja chumba alichokuwa amefikia, hadi mwanamke mmoja baada ya kushindwa kuvumilia kipigo alipowaambia wanajeshi hao chumba nilichokuwa nimefikia.
Bobi amesema alikataa kufungua mlango, ndipo wanajeshi hao walipoamua kutumia chuma kizito kuvunja mlango, na walipofanikiwa walimuamuru anyooshe mikono juu na kisha alianza kushambuliwa na wanajeshi wapatao sita wengine wakimgonga kichwani na usoni na chuma hicho kizito kichwani.
Bobi amedai kuwa kabla ya kuingia kwenye hoteli hiyo ndio wanajeshi hao walianza kushambulia gari lake kwa risasi ambapo walifanikiwa kumuua dereva wake aitwaye Yasin ndipo watu wake wanaoendesha mitandao ya kijamii akawashauri waposti picha ya tukio hilo kupitia Twitter.
Akiendelea kusimulia tukio hilo, Bobi amesema alipokamatwa alifungwa miguu na mikono kisha kufungwa kitambaa cheusi usoni na akastuka yupo katika kambi ya jeshi.
Amesema aliwekwa kwenye chumba kidogo ambapo ameeleza kuwa alipigwa ikiwemo kutolewa kucha na kutobolewa masikio na kitu chenye ncha kali ambapo maumivu yake hawezi kuyaelezea.
Amedai pia hakula kwa siku tatu hadi tarehe 16 Agosti alipokuja kutembelewa na mkewe pamoja na mdogo wake hospitalini alikokuwa akipatiwa matibabu.