Bocco Kuikosa Mechi ya Yanga

Simba Yapata Pigo Bocco Kuikosa Mechi ya Yanga
Furaha ya mabao mawili aliyoifungia Simba dhidi ya Mwadui, ilimalizika kuwa kilio kwa nahodha John Bocco, baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu itakayomfanya akose mechi ya watani wa jadi dhidi ya Yanga, Septemba 30 jijini.

Bocco alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 81 na mwamuzi Alfred Vitalis wa Kilimanjaro, baada ya kumpiga ngumi ya kisogo beki wa Mwadui, Revocatus Mgunga.

Awali, Mgunga alimchezea madhambi mshambuliaji huyo nguli, alipokuwa kwenye harakati ya kuokoa shambulizi lililokuwa linaelekezwa langoni mwake.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, Bocco atakosa mechi tatu zinazofuata ikiwemo dhidi ya Yanga na huenda adhabu hiyo ikaongezeka kutokana na kosa alilofanya kuwa sio la kiungwana.

Msimu uliopita Mgunga ndiye aliyemchezea madhambi Bocco katika mechi ya mzunguko wa kwanza na kumsababishia majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja muda mrefu.

Mechi ya jana ilitawaliwa na matukio yasiyofurahisha na yanayovutia kwa Bocco kwa kuwa mbali na kadi hiyo nyekundu, mabao yake mawili yalitoa mchango mkubwa kwa Simba kushusha presha baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo miwili mfululizo dhidi ya Ndanda na Mbao FC ambapo ilipata pointi nne, ikifungwa moja na kutoka sare moja.

Bocco amefikisha jumla ya mabao 100 katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo amefunga katika timu mbili tofauti Azam na Simba.

Hata hivyo, kadi nyekundu ya Bocco haikuweza kuizuia Simba kuibuka na ushindi mnono wa ugenini wa mabao 3-1 ambao umeifanya kufikisha pointi 10 na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kabla ya mchezo wa jana usiku baina ya Yanga na Singida United.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad