Bonde la Msimbazi Kugeuzwa Kivutio cha Utalii


Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo amesema serikali inaendelea na mazungumzo ili kupata dola za Kimarekani milioni 60 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa bonde la Msimbazi ambao unatarajiwa kumaliza tatizo la mafuriko na uharibifu wa miundombinu.


Waziri Jafo ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akihitimisha ziara ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa uboreshaji na uendelezaji wa jiji hilo.

"Mradi huu kwa ujumla unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 80 lakini hadi sasa tayari tumeshapata dola milioni 20, na utakapokamilika utawezesha magari kupita muda wote hata kipindi cha mvua. Tukipata dola milioni 60 ndoto zetu za kulifanya eneo hili kuwa kivutio cha utalii badala ya kuwa kero kwa wananchi zitatimia", amesema Jafo. 

Aidha, Jafo ameeleza kuwa, kukamilika kwa mradi huo pia kutatatua tatizo la magari ya mwendokasi, kushindwa kutoa huduma kipindi cha mvua na kwamba jukumu lao kama viongozi ni kufanya maamuzi sahihi.

"Matamanio yetu ni kwamba, kabla serikali ya awamu ya tano haijaondoka madarakani ndoto za mradi huu ziwe zimetimia na tunamini litaleta matokeo makubwa. Tunatamani pia jambo hili mwakani liingie kwenye bajeti yetu. Kutoka sakafu ya moyo wangu natamani mambo haya mazuri ambayo wadau wamepoteza muda wao kuyaandaa tuweze kuyatekeleza. Takriban miezi tisa ya uchambuzi sasa  tumeweza kupata majawabu Msimbazi ikoje na inahitaji nini, sasa tutoke katika makaratasi twende katika utekelezaji" ,amesisitiza Jafo.

Kukamilika kwa mradi huo kutaweza kuleta faida nyingi kwa wananchi, pamoja na usafiri wa mwendokasi kufanya kazi zake ipasavyo hasa nyakati za mvua bila ya kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuhofia mafuriko yanayotokea eneo hilo pindi mvua zinaponyesha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad