Khan amesema kuwa yeye kwa hivi sasa anafahamika ulimwengu mzima kwa sababu ya mafanikio aliyopata katika mapambano yake ya Marekani, wakati bingwa huyo wazamani wa dunia uzito wa light-welterweight akiwa amepambana zaidi ya mapambano 10 huko Las Vegas na New York Madison Square Garden.
Mwanamasumbwi huyo amesema King Joshua ambaye anatarajia kushuka ulingoni hapo kesho siku ya Jumamosi kutetea mkanda wake dhidi ya Alexander Povetkin kwenye uwanja wa Wembley ulimwengu mzima ungemfahamu kama angezipiga Mmarekani na kuachana na tamaduni za kupigana mapambano yake England.
“Ndiyo, kama unahitaji kuwa nyota wa ulimwengu mzima ni lazima uwende ukapigane Marekani, ndoto zangu ilikuwa kupigana Las Vegas, Madison Square Garden maeneo ambayo Muhammad Ali na Mike Tyson wamepata kupigana,” amesema Khan.
Khan ameongeza “Kivyovyote vile litakavyo onekana Marekani basi huonekana dunia nzima, nilianza kuwa na jina kubwa baada ya kupambana Marekani.”
“Watu wa Pakistan walianza kunifahamu, wakati nilipo pigana pambano langu la kwanza England hakuna aliyenijua Pakistan lakini wao na India walianza kunifahamu baada ya pambano langu kufanyika Marekani ukweli ni kuwa ukipambana Marekani hukufanya wewe kuwa maarufu ulimwenguni.”
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 31 ambaye anatarajia kupambana na mkongwe, Manny Pacquiao Desemba 8 mwaka huu anaimani kuwa Joshua angetengeneza mkwanja mrefu zaidi kama pambano lake lingefanyika nchini Marekani.