Canelo ‘Saul’ Alvarez ametangazwa kuwa mshindi wa pambano kati yake na Gennady ‘GGG’ Golovkin lililomalizika dakika chache zilizopita.
Majaji wa pambano hilo la marudiano wametoa matokeo ambayo yanaonesha kuwa majaji wawili wamempa Canelo ushindi wa raundi mbili mbele ya Golovkin (115-113), huku jaji mmoja akiamua kuwa ilikuwa sare (114-114).
Matokeo hayo yamemtawaza Canelo kuwa bingwa mpya wa dunia uzito wa kati wa WBC/WBO na kumfanya kuwa na rekodi ya kushinda mapambano 50, kushindwa moja na kutoa sare 2.
Matokeo haya pia yanaweka alama kwenye rekodi ya Golovkin ya kupoteza pambano kwa mara ya kwanza kati ya mapambano 40 akiwa na sare moja.
Kupitia mitandao ya kijamii, tayari umezuka utata mkubwa wa matokeo hayo, wengi wakiamini kuwa ilikuwa ni sare nyingine au huenda Golovkin alishinda kwa raundi moja mbele ya Canelo.
“Ni dhahiri kuwa kambi ya GGG lazima itakasirishwa na tangazo la matokeo haya, lakini kwakweli lilikuwa pambano la ukaribu sana (close fight),” imeandika Washington Post.
Mashabiki wengi kwenye mtandao wa Twitter waliwavaa watangazaji wa pambano hili kupitia HBO, wakidai kuwa walikuwa wanatangaza kwa kumpendelea Canelo.
“Ni kama wanachotangaza ni pambano tofauti kabisa na tunachokiona. Wanalazimisha Canelo awe ametawala,” inasomeka moja ya Tweets.
Mashambulizi hayo ya mashabiki dhidi ya HBO, yalikifanya kituo hicho kujibu kwa kuweka kwenye Twitter picha inayowaonesha wawili hao baada ya pambano na kuandika, “inasema yote.” Lakini ni kama walichochea kushambuliwa.
Pambano hili la marudiano lililenga kumaliza ubishi wa pambano la awali la Septemba mwaka jana lililomalizika kwa sare ambayo ililalamikiwa zaidi.
Hata hivyo, ni kawaida kwa mapambano makubwa kuwagawa mashabiki na watalaam wa masumbwi hasa linapokuwa pambano ambalo wapiganaji wanazidiana kidogo.