Dah! “Ningekuwa mbali sana kimaisha vijana wenzangu niliosoma nao sasa wana maisha mazuri baadhi wanafanya kazi benki, bandarini na wengine wapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ingawa darasani hawakuwa vizuri kama nilivyokuwa.” Hayo ni maneno ya Jonas Kessy.
“Kuanzia shule ya msingi hadi sekondari nilikuwa nawaongoza kimasomo…kwa kweli sikio la kufa halisikii dawa, sikutaka kupokea ushauri kutoka kwa ndugu wala jamaa zangu, niliambatana na makundi yaliyoniingiza kwenye utumiaji wa dawa za kulevya.”
“Kwa kweli sijisifu lakini kimasomo nilikuwa nawaongoza wanafunzi wenzangu kama mtihani wa kumaliza elimu ya msingi nilikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora kitaifa kwa kushika nafasi ya tatu huku kwa Mkoa wa Arusha nikishika nafasi ya kwanza.”
Matokeo ya Kessy katika mtihani wake wa Kidato cha Nne ni; Mathematics-A, English-A, Geograph-A, History-A, Kiswahili-A, Civics-B, Biology-B.
Kessy ambaye ni mhamasishaji wa taasisi ya kusaidia vijana wanaotumia dawa za kulevya ya Dunia Moja Pamoja, anaeleza kuwa alianza kutumia dawa za kulevya mwaka 1998 akiwa darasa la nne katika Shule ya Msingi Green Acres ambapo anasema wakati huo alianza kuvuta bangi.
“Nikiwa darasa la nne nilijiunga na makundi ambayo kwangu hayakuwa sahihi. Baadhi ya watu niliokuwa nikiongozana nao wengine walinizidi umri, hivyo walikuwa wakinilazimisha nijaribu kuvuta bangi pindi nilipokuwa nao.
“Unajua tena ujana ni maji ya moto kila kitu ukipewa unajaribu ili uonje ladha. Wenzangu nilipoongozana nao wote walikuwa wanavuta bangi,” anasema.
Kessy anasema, “wakaanza kwa kunilazimisha lakini baadae nilizoea na kuwa miongoni mwa wateja wa kilevi hicho, nilipokosa bangi ilikuwa lazima niende vijiweni inakopatikana. Nikaendelea kuvuta bangi hadi nilipomaliza darasa la saba.”
Anasema bangi ilimwingia hakuweza kuacha japo alijitahidi kuachana nayo, lakini ilishindikana kutokana na ushawishi alioupata katika makundi aliyokuwa akiongozana nayo.
Kessy anasema alifanya vizuri katika mitihani yake ya kumaliza elimu ya msingi ambapo alishika nafasi ya tatu kitaifa na alichaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari ya Elboru, Arusha.
Aanza kutumia heroine, udokozi
Anasema akiwa shuleni hapo awali aliendelea kuvuta bangi, lakini akiwa katika harakati za kusaka dawa hiyo ya kulevya akakutana na watumiaji wa dawa nyingine aina Heroin, naye akashawishika kuanza kuitumia.
Kwa mujibu wa Kessy, alipojiingiza kwenye uvutaji wa heroine ndipo alipoanza kubadilika na kuwa na tabia za udokozi kwa kuiba vitu vidogo vidogo na kuviuza ili apate fedha kwa ajili ya kununulia unga huo.
Kessy anasema aliendelea na wizi huo ambapo wakati mwingine aliwaibia wanafunzi wenzake chochote alichokuwa akikiona mbele yake ilimradi apate fedha kwa ajili ya kununulia dawa za kulevya.
Hata hivyo, Kessy anasema hadi wakati huo bado alikuwa vizuri kimasomo ambapo anamshukuru Mungu alikuwa na uwezo wa kuelewa darasani na katika matokeo ya kidato cha nne alipata daraja la kwanza (I.9) na kuchaguliwa kujiunga Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari ya Kibaha iliyoko wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Anaelezea akiwa kidato cha tano alizidisha kuvuta dawa za kulevya ikafikia wakati aliacha kwenda shule akawa anashinda Maili Moja (Kibaha) kwenye vijiwe vya dawa hizo na kwamba hapo ndipo alipobadilika, alianza kuwa mchafu huku akizidisha vitendo vya wizi, kupora mikoba ya wanawake na kuiba vitu mbalimbali ili wapate hela kwa ajili ya kununulia heroin.
Kessy anasema baada ya kuwa haonekani shuleni, aliandikiwa barua ya kufukuzwa shule na kulazimika kurudi nyumbani.
Kwa kuwa alizoea kuvuta dawa za kulevya alianza kuiba vitu vya nyumbani kwao na alifikia hatua ya kuuza hata nguo zake anazovaa ili pate fedha.
Anasema siku ambayo hatoisahau katika maisha yake ni pale alipoiba kifaa cha gari (Power Window) eneo la Dar Free, Kinondoni ambapo alipigwa hadi kupoteza fahamu kwa siku tatu, alipozinduka alijikuta yupo hospitali ya Mwananyamala.
Baada ya kutoka hospitalini alianza tiba katika kitengo cha Kinga na Tiba ambapo alikuwa akipewa vidonge vya Methadone ili kumponya na uvutaji wa dawa za kulevya. Hata hivyo, anasema alipokuwa akitoka kunywa dawa hizo alikutana na wezake na kuendelea kutumia heroin.
Anaeleza kuwa ndugu zake walimpeleka hospitali mbalimbali za kutibu magonjwa ya afya ya akili ikiwemo Lutindi iliyopo Korogwe mkoani Tanga, Highdom iliyoko Mbulu mkoani Manyara na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), lakini ilishindikana kupona.
Anasema alipokuwa akiruhusiwa kurudi nyumbani aliendelea kutumia dawa za kulevya ambapo alifungwa jela mara kwa mara lakini haikumsaidia chochote katika kukabiliana na utumiaji wa dawa hizo.
“Kumkamata aliyeathirika na dawa za kulevya na kupelekwa jela siyo fundisho. Mfano ni mimi nilikuwa nafungwa na nikiachiliwa nilikuwa naendelea kuvuta dawa za kulevya.
“Nilichotakiwa kupewe ni elimu ya kujitambua ili niachane na uvutaji wa dawa za kulevya na siyo kutumia nguvu, kunilazimisha niache kwa kunipeleka jela haikuweza kunisaidia bila ya elimu ya kutosha kuhusiana na tatizo hilo,” anasema Kessy.
Anasema licha ya kuachana na utumiaji dawa za kulevya bado anakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya jamii inayomzunguuka kumuogopa kutokana na historia ya maisha aliyoyapitia na kumfanya akose kuaminiwa pindi anapokwenda kuomba kazi hali aliyosema imekuwa ikimtesa kisaikolojia.
Kessy anasema hadi sasa jamii na baadhi ya ndugu zake wa karibu hawamuamini pindi anapowatembelea wakidhani anaweza kurudia tabia yake wakati huko alishaondoka na kuacha vitendo hivyo.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Saida Kessy aliyewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1997, anasema Jonas ambaye ni mdogo wake wa mwisho katika familia yao, alianza kupata elimu kutoka kwenye taasisi zinazosaidia watu walioathirika na dawa za kulevya (sober) ndipo alipobadilika na kuacha kabisa kutumia kilevi hicho.
“Nakumba siku tatu za mwanzo alipokuwa akicha dawa za kulevya aliumwa sana, aliharisha hadi tulihisi labda ana malaria kumbe yawezekana sumu ilikuwa ikitoka mwilini mwake lakini baada ya hapo aliendelea vizuri.
Kamishna wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Dk Peter Mfisi, anasema wanatoa elimu ya ushauri pamoja na dawa za Methadone kwa walioathirika na dawa za kulevya.
Dk Mfisi anasema kutokana na udhibiti mkubwa wa dawa za kulevya unaofanywa na mamlaka yake kwa kushirikiana na vyombo vingine, watumiaji wa dawa hizo sasa hawazipati kama ilivyokuwa awali na kama wanazipata hulazimika kuzinunua kwa bei kubwa.
Anasema kwa kukosa dawa za kulevya waathirika wamekuwa wakipata maumivu makali matokeo yake wengi wao hukimbilia kwenye vituo hivyo ili waweze kupatiwa matibabu.
Dk Mfisi anasema mpaka sasa waliosajiliwa kwenye kitengo cha kinga na tiba wamefikia zaidi ya watu 6,000 wanaotumia dawa za Methadone.
Anasema hadi sasa vituo vinavyotoa huduma hiyo vipo vitano mbavyo vinapatikana katika hospitali ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliyoko mkoani Mbeya, Hospitali ya Sekou Toure, Mwanza, Hospitali ya Mwananyamala, Temeke na Muhimbili zilizopo Dar es Salaam.
“Vituo vilivyopo havitoshi vimeelemewa na watu wengi walioathirika na dawa za kulevya wanajitokeza ili kupatiwa matubabu, hivyo sasa tunataka kuanzisha vituo vidogovidogo maeneo ya pembezoni wanakotoka waathirika mfano Mbagara, Buguruni na Kigamboni,”anasema Dk Mfisi.
Anasema lengo lao wanapowatibu waathirika wa dawa za kulevya ni kuhakikisha akili zao zinarudi kama mwanzo na kuacha kutumia dawa hizo. “Hata kama bado hawajakaa sawasawa wanapoendelea na tiba wanakuwa wasafi, wanaacha wizi na wanafanya kazi”.
Pia, anasema kitengo hicho huwapima magonjwa mengine yanayoambatana na dawa za kulevya kama Kifua Kikuu, magonjwa ya ini na yale ya zinaa ambapo wakibainika kuwa na tatizo lolote hupatiwa tiba.
Kamishna wa Operesheni DCEA, Luteni Kanali Fredrick Milanzi anasema wanaendelea kuwabana wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya ili kuhakikisha haziingii nchini.
“Kwa sasa hawapitishi hapa dawa za kulevya wanachofanya wanazipitishia kwenye baadhi ya nchi zikiwemo za jirani wakihofia kukamatwa,” anasema Luteni Kanali Milanzi.
Luteni Kanali Milanzi anasema huko nyuma dawa za kulevya zilikuwa zikiuzwa hadi kwenye vituo vya daladala, lakini sasa hata waathirika wa matumizi ya dawa hizo ‘mateja’ ambao walikuwa wakionekana kila kona wameanza kuadimika, wengi wanatumia tiba baada ya kukosekana kwa ‘unga’.