Wananchi wa Kijiji cha Ukami katika Kata ya Mapanda, Tarafa ya Kibengu wametoa malalamiko yao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kwa kudai kudhalilishwa na Mganga wa Mkuu wa Kitucha Afya cha Ukami, Dk. Andrew Kitwanga, hali iliyosababisha mganga huyo kusimamishwa kazi.
Wananchi hao walidai daktari huyo huwatoza faini ya shilingi 50,000/- endapo wakichelewa kufika kupata huduma na kuwapa adhabu za kufagia uwanja wa kituo cha afya na kudeki vyoo ndipo yeye aweze kuwatibu.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa Hapi kwenye mkutano wa hadhara uliofanika kijijini hapo wiki iliyopita, wananchi hao walidai kuwa wagonjwa na wanaoongozana na wagonjwa kwenda kuwauguza nao pia wanayanyaswa na daktari huyo.
Walidai kuwa mara nyingi daktari huyo amekuwa na kauli chafu kwa wagonjwa na kushindwa kuwapa matibabu sahihi na yanayotakiwa huku akijua kuwa wananchi ndio waliojenga majengo hayo kwa nguvu zao. Wananchi hao walidai kuwa wanawake wenye watoto wanalazimika kukimbia huduma za kituo hicho na kulazimika kuzalia nyumbani kukwepa faini wanayotozwa na adhabu za kuosha vyoo anazotoa daktari huyo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Hapi baada ya kusikiliza malalamiko hayo alimsimamisha kazi daktari huyo kutokana na alichodai kufanya hujuma na kuwanyanyasa wagonjwa kinyume na sheria na taratibu za afya kama zinavyotakiwa. Alisema kuwa hatawafumbia macho watumishi wa Serikali wanaokiuka sheria na taratibu za kazi wakati Serikali imewasomesha kwa gharama kubwa na badala yake wanajichukulia kazi hizo kama za kwao binafsi.
Amewataka watumishi wa Serikali katika nyanja tofauti tofauti kuhakikisha kuwa wanaheshimu sheria na taratibu za kazi kama zilivyowekwa na Serikali na utaalamu waliosomea kwa kuhakikisha kuwa wanaleta mafanikio yenye tija kwa taifa na Serikali yao na kuhakikisha kuwa wanaondoa kero ambazo zinawasumbua wananchi katika maeneo yao.