DNA yatambua mwili uliozikwa


MWILI mmoja kati ya minne iliyokuwa haijatambuliwa na ndugu zao na kuzikwa juzi kitaifa katika makaburi ya pamoja kisiwani Ukara, eneo la Bwisya, umetambuliwa baada ya vipimo vya vinasaba (DNA) kushabihiana na binti yake.

Mazishi hayo ya pamoja yaliongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, juzi. 

Mwili huo ulitambuliwa na ndugu zake baada ya serikali kujiridhisha kwa kupima vinasaba vya binti wa marehemu ambaye alifuata taratibu za kisheria. 

Akizungumzia utaratibu uliotumika, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Walemavu, Jenista Mhagama, alisema ndugu wa marehemu akiwamo mume na watoto wake wa kike wawili, walifika kutoka mkoani Kagera katika Wilaya ya Muleba, Septemba 24 na kujitambulisha, lakini kulingana na maelekezo ya rais na sheria husika, ilibidi uhakiki ufanyike. 

"Ndugu hawa walifika na kudai marehemu huyo alikuwa ndani ya kivuko hicho, sisi tulielekeza wataalamu husika vikiwamo vyombo vya dola ambavyo vinahusika katika maafa haya, mahojiano yalifanyika kwa takribani saa tatu na upimaji wa DNA ulifanyika hadi kubaini mwili wa marehemu ambaye ndugu zake walisema anaitwa mama Muleba ulikuwa ni halali wapewe," alisema Mhagama. 

Aidha, Mhagama alisema ndugu wa mama Muleba walitaka mwili huo ufukuliwe waende wakazike wenyewe, lakini kulingana na familia hiyo ilivyoshauriana, waliridhia uachwe hapo katika eneo la Bwisya kisiwani Ukara. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, aliwataka Watanzania wote ambao wanajua ndugu zao walikuwa katika kivuko hicho wajitokeze ili kuweza kupima DNA hatua ambayo italeta faraja kuona kila aliyefariki katika kivuko cha MV. Nyerere ametambulika na ndugu wamefahamu mahala alipozikwa. 

Aidha, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema mwili mmoja umepatikana jana na kufanya idadi ya waliokufa maji kuwa 228 huku fedha za michango inayotolewa kwa ajili ya rambirambi iliyokusanywa ni Sh. 557,020,000. 

Katika michango hiyo Benki ya KCB ilitoa Sh. milioni 125, ambayo iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Benki hiyo, Zuhura Muro, ambaye alisema kufuatia ajali hiyo Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa KCB Tanzania, wanaungana na Rais Magufuli katika kuomboleza msiba huo mkubwa uliotokea kwa wananchi wa Ukara na Tanzania kwa ujumla, huku Kanisa Katoliki kupitia Askofu Flavian Kassala, likiwakilisha rambirambi ya Kanisa la Jimbo Kuu la Dar es Salaam, iliyotolewa na Kadinali Polycarp Pengo Sh. milioni 25. 

Naye Mkuu wa Majeshi nchini (CDF) Venance Mabeyo, alisema kazi ya kukiondoa kivuko cha MV. Nyerere ndani ya maji iko katika hatua nzuri baada ya kukipindua kutoka kifudi fudi na kuwa katika hali ya ubavu kutokana na juhudi za vikosi vya uokoaji vilivyopo eneo hilo na kuleta matumaini ya kumaliza kazi hiyo mapema. 

Kwa mujibu wa Mhasibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Henry Kilenga, ambaye  anafanya kazi ya kutoa fedha hizo, alisema idadi ya ndugu wa marehemu wa ajali ya kivuko cha MV. Nyerere waliojitokeza kuchukua fedha hadi jana walifikia 127. Kila mmoja alikuwa akipewa Sh. milioni moja. 

Naye Kenned Ogutu, ambaye alimpoteza binti yake wa kazi na mke wa marehemu mdogo wake katika ajali hiyo, alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wananchi ambao wamefikwa na maafa hayo. 

Alisema msiba huo ulikuwa wa ghafla na  ingewawia vigumu kama wasingepata msaada kutoka kwa serikali na Watanzania. 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad