Mwenyekiti wa Chama cha CHAUMA, Hashimu Rungwe amesema sera ya elimu bure inapaswa kwenda sawa na wanafunzi kula chakula shule pamoja na kupata vifaa vya shule ikiwemo vifaa vya kufundishia kama maabara.
Rungwe amesema ili kuweza kupata kizazi kilicho na maarifa na msaada kwa Nchi inapaswa kuwepo na kundi kubwa la wasomi lakini kama wanafunzi wanapewa elimu bure bila chakula basi litakua jambo gumu kuona wakifaulu katika mitihani yao.
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020, Rungwe amesema watafanya siasa kama kawaida kwa kunadi sera zao kwa wananchi ambao wataamua ni nani ambaye wanaona atawafaa kwa ajili ya kuwatumikia.
" Sisi ni wanasiasa, tutafanya siasa unatarajia kuona mimi nacheza mpira? Tutafanya siasa tu na siwezi kusema watanzania watarajie nini hakuna mtu anaesema silaha zake, wataziona wakati ukifika,"
" Unaweza kusema umefanya shule bure lakini mwingine atatekeleza zaidi, Rais ana wajibu wa kutekeleza ndo kazi yake, mtu akifanya kazi unamuacha, hakuna kupiga kelele sijui Baba kaja na samaki, Baba kanipa gari, wewe ushawahi kuona wapi?" amesema Rungwe.