Ninapo taja masoko makubwa ya nguo za ndani za mitumba, hapa nazungumzia Mwenge, Ilala, Tandika na hata Manzese.
Wanawake ndio watumiaji wa kubwa kwani kwa upande wa wanaume nguo zao kubwa za ndani ni kaoshi, soksi na taiti.
Lakini kwa upande wa wanaweke hupendelea zaidi kutumia sidiria, nguo za kulalia, taiti na hata chupi.
Nguo hizi za ndani za mtumba, hupendwa zaidi kwasababu baadhi husema ni imara na zina dumu lakini pia hupatikana kwa bei raisi sana, zingine huuzwa miatano au elfu moja na zipo za mpaka elfu kumi na zote ni za mtumba.
Pamoja na urahisi huo, watumiaji wanafahamu nini juu ya madhara ya kuvaa nguo hizi za ndani zilizo valiwa na watu wengine ambao hatuwajui? Hatujui afya zao na wala magonjwa ambayo huenda wanayo.
BBC imezungumza na baadhi ya watumiaji wa nguo hizo za ndani baadhi wanaonyesha kuto jua lolote kama yanaweza kuwepo madhara.
"Mi hayo madhara hata siyajui ila napata zangu nguo kwa bei poa na napendeza kama kawaida. Kama kuna madhara haya," anasema bi Aisha wa soko la karume.
Hata hivyo Ally Saleh mtumiaji wa nguo za ndani za mitumba anasema yeye huangalia zilizo mpya mpya.
"Mimi huwa nachukua ule mtumba wa grade A na zangu zinakuwa mpya mpya hazijatumika sana, ila kuhusu madhala labda zile zilizo chakaa kupita kiasi. Mie singlendi zangu ata boksa napata kali mtumbani," Ally anaiambia BBC.
Wengine wanafurahia ubora hali inayopelekea kufumbia macho juu ya elimu waliyo nayo.
"Mie naambiwa tu kwamba zina madhara lakini ukiziona zinaonekana bora na nzuri kuliko za dukani yaani ukivaa sidiria ya dukani inafanya matiti yanakuwa mama ni bebe, wakati ya mtumba kwa raha zangu kitu talk to me inakamata muruaa," Nola Almasi anaiambia BBC.