Championi Ijumaa likiwa nchini Uganda hivi karibuni, likifanikiwa kukutana uso kwa macho na mfanyabiashara huyo na kumdadavua kwa namna yake ambapo alibainisha namna anavyoendesha shughuli zake ikiwa sabamba na suala zima la michezo.
Huyu hapa anafungukia ishu nzima: “Watu wengi wananijua kama Jack Pemba, ambaye nimezaliwa Februari 5 mwaka 1973 nchini Tanzania ndani ya Dar es Salaam, kwa sasa nipo hapa Uganda kwa takribani miaka 10, ambapo niliondoka Tanzania mwaka 2007 baada ya kufeli kile ambacho nilitaka kufanya kwa kusaidia michezo, hivyo nikalazimika kuhamishia makazi yangu katika Mji wa London, Uingereza ambapo mambo yangu yalianza kunyooka. “Lakini nilipoanza safari ya kurudi Tanzania niliamua kupita hapa Uganda ambapo nilianza harakati zangu za kuisaidia michezo na hatimaye nilifanikiwa vya kutosha.
Kwa sasa unafanya nini? “Sasa hivi niko na timu ya mpira wa kikapu kwa wanaume (basketball) nimedhamini timu ya taifa ya Uganda, nimegawa mipira katika shule zote za serikali, nimesaidia timu ya Olympic Lion kuipeleka katika mashindano ya mwaka 2016, nimefanya mengi ambapo ukienda kwenye Google utaona ni kwa kiasi kipi nimeweza kufanikiwa sana kuhusu hili.
Rais Museveni ndiyo msaada wake “Tangu nijikite kwenye michezo, nilibahatika kupata sapoti kubwa kutoka kwa Waziri wa Michezo hapa Uganda pamoja na Rais Yoweri Museveni kwa ushirikiano mkubwa na wananchi wa hapa Uganda. Mali unazoonyesha mitandaoni ni zako zote?
“Kila kitu unachokiona ni mali yangu halali jambo ambalo linanifanya saa nyingine watu wenye nia mbaya kutaka kunivurugia njia zangu za utafutaji na uendelezaji wangu wa michezo kwani kama uliona hapo nyuma kidogo, kuna watu wahuni ambao wanaishi hapa wamekuwa hawafurahishwi na jinsi nilivyo na uhusiano mzuri na Rais Museveni.
“Katika mafanikio siku zote huwezi kufurahiwa na kila mtu ingawa mimi napendwa sana hapa Uganda, lakini utaona wahuni hao walinifanyia vitendo vya kashfa ila hawakuweza kufanikiwa. “Hata kipindi naanza harakati zangu za kujiweka sawa katika michezo baadhi ya vyama vya michezo vilijaribu kuleta fitina za hapo na pale, kwa nguvu ya Mungu walishindwa na ndiyo maana nimeendelea kushika chati na kuzisaidia timu nyingi za mchezo wa mpira hapa nchini.
“Ile skendo ya kwamba nimefilisika haikuwa na ukweli wowote kwani magari yote yaliyoonekana nayauza yalikuwa ni mali yangu lakini niliamua kuyauza japo kuna mtu ambaye alitaka kunizunguka kwa nia ya kunitapeli ila serikali ikanisimamia kikamilifu nikamshinda mahakamani na kila sehemu.
“Mtu huyohuyo na baadhi ya watu wengine wakajaribu kwa njia nyingine ambazo mnazielewa siwezi kuziongelea hapa sijui mambo ya ‘sex tape’ kitu ambacho nilikuwa siyo mimi na wala siwezi kufanya huo ujinga, mimi ni Mganda na Mtanzania ambaye nimefanikiwa zaidi kwenye biashara za michezo pamoja na zingine zinazoniingizia kipato ambazo ni za utalii na zile za kuleta wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza nchiniUganda. Lini Watanzania watakuona tena katika nchi yao?
“Natarajia kurudi nyumbani mwezi ujao kuja kusaidia na kuendeleza mpira wa miguu, nimefurahi sana na nimekaribishwa tena na TFF (Shirikisho la Soka la Tanzania) wameniambia nirudi tena na ninaweza kufanya kazi na wao kwa mara nyingine tena kwa mkataba ambao siyo wa kuvunja sheria na Katiba ya TFF ili tuweze kuuendeleza mchezo wa soka na imani nikishafika tutaweka kila kitu pamoja.
Kitu gani ambacho unawaambia Watanzania? “Jina langu ni Jack Pemba na nimefanikiwa zaidi kuliko huko nyuma nilipokuwa Tanzania na sasa hivi mimi ndiye tajiri wa kweli kuliko yule wa Tanzania, Mungu ambariki Rais Magufuli kwani ndiyo rais wangu bora kuliko wote Afrika Mashariki.
“Ninarudi kuhakikisha namsaidia katika kufanikisha suala la michezo kwani hapa tayari nishamaliza na Rais Museveni ananijua, waziri wa michezo ananijua nishafanya vitu vingi sana katika nchi na sasa narudi Tanzania,” anasema Pemba.
MAKANA NA MUSA MATEJA