Kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella imeahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi Septemba 24, mwaka huu.
Ni baada ya Wakili wa Serikali, Patrick Mwita leo Septemba 12, kueleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa lakini jalada lililikuwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wiki mbili zilizopita.
Mwita aliiomba mahakama iipangie kesi hiyo tarehe ya kutajwa ili aweze kufuatilia jalada la kesi hiyo lipo wapi kwa sababu Makao Makuu ya ofisi ya DPP yamehamia Dodoma hivyo ni lazima awasiliane nao.
Baada ya kueleza hayo,Hakimu Simba alimwambia Wakili huyo Septemba 24 mwaka huu atoe majibu kwa mahakamani.
Katika kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2017, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua kwa makusudi dada wa marehemu bilionea, Erasto Msuya, Aneth Msuya.
Tukio hilo, linadaiwa kufanyika Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Washtakiwa hao, awali Februari 23, 2016, waliachiwa huru katika kesi ya mauaji namba 32 ya mwaka 2016 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mwambapa.
Baada ya kufutwa kwa kesi hiyo iliyokuwa ikifanana na hii walikamatwa na baadaye kusomewa upya mashtaka hayo ya mauaji.