Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amesema kupishana kauli baina yake na watendaji wenzake hujitokeza pale tu wanapozungumzia namna nzuri ya kuwaletea maendeleo wananchi wanaowaongoza na si vinginevyo.
Muro alitoa kauli hiyo jana baada ya kuibuka kwa mijadala hasa mitandaoni inayotokana na vipande vya video vinavyomwonyesha akimfokea mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Meru, Emmanuel Mkongo na nyingine akichana hotuba aliyokuwa ameandaliwa.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wanasema, kuna mambo hayapaswi kufanywa hadharani bali viongozi kuyamaliza katika vikao vya ndani ili kuwa na utawala unaoheshimiana.
Muro ameonekana katika kipande cha video akimfokea Mkongo mbele ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, jambo lililozua mjadala huku yeye (Muro) akisema, “ukiwa kiongozi wewe ni jalala, uchafu wote utakuhusu lakini mazuri hawayasemi.”
Anaonekana akisisitiza kuwa hatavumilia tabia ya kukaa kumsubiri mkurugenzi huyo kwa zaidi ya dakika 10. “Huu ni upuuzi sitauvumilia, usicheke mkurugenzi, usinidharau mimi,” anasema Muro mbele ya Gambo katika video mmojawapo.
Muro aliwahi pia kuchana hotuba aliyopewa na watendaji wa Wilaya ya Arumeru alipofanya mkutano nao kwa madai ni upuuzi na haina kitu. “Nimepewa hii (hotuba) haina kitu ina kupongeza tu ooh... tunafuata sheria ya namba sita ya mwaka 2013 ambayo mimi ipo kichwani, ona naichana,” alisema kwenye mkutano huo.
Hivi karibuni katibu mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mussa Iyombe akizungumza na wakuu wa wilaya 26, alisema miongoni mwa sababu za kutenguliwa kwa uteuzi wao ni kutojiheshimu.
Alisema wakuu wa wilaya wengi walioondolewa ni kutokana na kugombana na wabunge au wakurugenzi wa halmashauri. “Unamnyang’anya gari dereva unaendesha wewe au wewe kazi yako ni kugombana tu na wabunge wakati una kazi zako na mbunge ana kazi zake,” alisema Iyombe.
“Niwaambie ukweli, wengi walioondoka ni kwa sababu hiyo. Sasa wewe kila siku unagombana na viongozi wenzako Serikali gani hiyo ambayo inagombana tu na wawakilishi wa wananchi.”
Katika mazungumzo yake na wakuu hao wa wilaya, Iyombe aliwataka wajiheshimu na kutunza heshima ya Rais John Magufuli kwa sababu ana imani nao na anakasirishwa na vitendo hivyo.
“Rais ana vyombo vingi vya kukuangalia wewe, hivyo mnatakiwa kuwa waangalifu kwenye hizi nafasi zenu. Niwaombe sana nyie muwe mfano, ikitokea mtumishi amekosea kuna mamlaka ya nidhamu, iagize tu usiende pale ukamweka ndani kwa sababu kuna sheria zinazomlinda huyo si mwanasiasa.”
Muro anasemaje?
Jana, Muro ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari akizungumza na Mwananchi alisema kutofautiana haimaanishi kwamba wana ugomvi. “Nikueleze tu, sina ugomvi na mkurugenzi wangu na sasa tupo ofisini tunafanya kazi,” alisema Muro huku akisisitiza kuwa katika kutafuta maendeleo ya wananchi, kutofautiana ni kawaida.
“Hizi ndizo changamoto za uongozi, hata viongozi unaowaona ni imara kwa sasa nao walikuwa na changamoto kama hizi.”
Kuchana hotuba
Kuhusu kuchana hotuba, Muro alisema aliichana alipokuwa kwenye kikao cha ndani baada ya hotuba hiyo kujaa sifa za kumsifia wakati alikuwa ndiyo amemaliza mwezi mmoja tangu ateuliwe. “Niliichana katika kikao cha ndani, nadhani aliyeisambaza kipande cha video ana malengo yake,” alisema.
Afundwa kiutendaji
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bakari Mohamed alisema kuwafokea watendaji hadharani kunashusha utendaji wao huku kikizaa kizazi cha watendaji wanaochelea kufanya uamuzi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alisema anachokiona ni kutokuwepo kwa mgawanyo halisi wa madaraka baina ya matawi mbalimbali ya utendaji ndani ya Serikali.