Jukwaa La Katiba (JUKATA) Lapinga Polisi Kushangilia Uchaguzi Kumalizika


Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limelitaka Jeshi la Polisi na tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na si kutumika kisiasa.

Kauli hiyo imetolewa jana Jumatano Septemba 19, 2018 na Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo amezungumzia hali ilivyokuwa katika uchaguzi wa Ubunge katika jimbo la Ukonga na Monduli pamoja na ule wa Udiwani katika kata 24.

Katika ufafanuzi wake Mwakagenda amesema amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya polisi kushangilia uchaguzi kumalizika salama wakati waliotakiwa kufanya hivyo ni wananchi.

"Polisi wanashangilia hadharani bila aibu kuwa uchaguzi umefanyika kwa amani kwani nani alitakiwa kuhakikisha kwamba amani hiyo inakuwepo si wao, wanashangilia ushindi upi wakati ni wajibu wao kulinda mali raia na mali zao”, alisema Mwakagenda.

Akiwazungumzia NEC, Mwakagenda alisema tume hiyo haipaswi kupendelea upande wowote wa chama cha siasa ili kuepuka kasoro ambazo hujitokeza katika chaguzi mbalimbali ikiwemo za marudio, "Uchaguzi ni kama mechi, tume ndio refa kwa hiyo kama itapendelea upande mmoja mechi haiwezi kuwa ya amani”.

Uchaguzi huo umefanyika Septemba 16, 2018 ambapo baada ya matokeo kutangazwa , Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam walipongezana hadharani kwa kulinda amani kabla na baada ya uchaguzi wa ubunge Jimbo la Ukonga, jambo ambalo katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole alilipinga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad