STRAIKA mkali kwa mabao ya vichwa, Meddie Kagere ambaye mtindo wa kushangilia kwa kufunika jicho moja umewafurahisha mashabiki amesisitiza kuwa yajayo yanafurahisha.
Kagere ambaye amecheza mechi mbili za ligi kuu ametupia mabao 3 huku bao 1 akifunga dhidi ya Prisons kwa guu lake la kulia na mabao 2 akifunga kwa bichwa dhidi ya timu ya Mbeya City ambao walilala na viatu.
Akizungumza na Spoti Xtra Kagere alisema kuwa kwake mtindo wa kufumba jicho ni mtindo wa kushangilia tu na kitu kikubwa ambacho kinafanya aweze kung’ara ni ushirikiano ndani ya timu.
“Tunacheza tukiwa ni timu na kwa kufuata maelekezo ya mwalimu tunafanikiwa kupata matokeo hivyo hicho ndicho kilicho nyuma ya mafanikio yangu ambayo ni ya timu kiujumla,” anasema mchezaji huyo mzaliwa wa Uganda aliyewaacha Gor Mahia kwenye mataa.
“Kuhusu mtindo wangu wa kuziba jicho ni aina tu ya ushangiliaji haina maana yoyote na ninaipenda kwa sababu tayari mashabiki wangu wameipokea vizuri, baada ya kupata matokeo mazuri kikubwa ni kutazama mbele kwa michezo yetu mingine,” anasema Kagere ambaye Yanga walimtaka lakini mkwanja ukapwaya.