Katibu Mkuu CCM "Hakuna Dar Es Salaam Ya Makonda"

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally Katika mwendelezo wa mahojiano aliyoyafanya na Raia Mwema, amemnyooshea kidole, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa namna anavyotekeleza majukumu yake ya ukuu wa Mkoa na kudai kuwa kulikuwepo udhaifu katika kushughulikia makontena kutokana na kufanya kazi bila kushirikishana.

Alieleza kuwa, Mkuu wa Mkoa alipaswa kuwashirikisha wenzake tangu hatua za awali, kwa kuwa Serikali ni moja, hakuna cha Waziri wala Mkuu wa Mkoa – wote ni Wateule wa Rais.

Bashiru alimnyooshea kidole Makonda kwa ubinafsi na kukumbushia jinsi ambavyo Mkoa wa Dar es Salaam ni mmojawapo ya Mikoa aliyoitaja hivi karibuni kwa kutotekeleza vyema Ilani ya CCM kutokana kufanya kazi bila ushirikiano.

“Hapa sina maana kwamba ni Mkuu wa Mkoa tu hapana, ni uongozi mzima chini ya Mkuu wa Mkoa na uongozi mzima chini ya Mwenyekiti wa Chama. Rais hawezi kwenda kuwafundisha uhusiano mwema, wao wenyewe ndio wanatakiwa kujua kwamba uhusiano mwema kikazi unamjenga zaidi kiongozi yeyote…”

Vilevile, Katibu Mkuu alimuonya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam juu ya tabia yake ya kuwaita wakazi wa Dar es Salaam, wananchi (Mkoa) wangu. “Na hii habari ya Dar es Salaam ya Makonda, hakuna Dar es Salaam ya Makonda, ni Dar es Salaam chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda.”

Bashiru aliongezea kuwa: “Kuna wakati namsikia anasema wananchi wangu, nani kamwambia anao wananchi wake? Hakuna wananchi wako. Hakuna kiongozi anamiliki wananchi, ni wananchi wenzangu.”

Aidha, Dk. Bashiru alikumbushia jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyowahi kuonya juu ya ubinafsi: …. mkianza kusema mimi – wewe au wao – sisi, hamfiki.

Hivyo, aliwaasa vijana wanaopewa uongozi wawe wanyenyekevu na kuacha papara kwani watapotea kama ambavyo vijana wengi waliowahi kuwa juu walipotea kwa kukosa unyenyekevu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad