Katibu Mkuu CHADEMA Awachana Wabunge Wanaohamia CCM


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo, CHADEMA, Dk. Vincent Mashinji, amesema, Wabunge na Madiwani wanaojiuzulu na kuhama chama, waondoke tu kwa wema wala hakuna haja ya kusuguana na kusumbuana kila kukicha. 

Dk. Mashinji ameweka wazi hilo leo kwenye mkutano wake na wanahabari jijini Dar es salaam, ambapo amesisitiza kuwa, mtu kuhama chama ni kutekeleza haki yake ya msingi ya Kikatiba na sio jambo la kusubiri usiku wa saa 6:00 ndio utangaze. 

''Kati ya Wabunge 73 tuliopata kwenye uchaguzi mkuu 2015, watatu ndio wamehama, lakini wanatangaza usiku wakati hakuna haja ya kufanya hivyo maana Mwenyekiti alishawaambia waondoke tu kwa wema na chama hakitahangaika nao'', amesema, Dk. Mashinji. 

Aidha, Dk.  Mashinji ameongeza kuwa wanaohama wangeiga mfano wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kupitia (CCM), Lazaro Nyalandu, ambaye alijiuzulu nafasi yake kwa kufuata utaratibu ikiwemo kumwandikia barua Katibu wa chama chake pamoja na Spika wa Bunge. 

Aidha, CHADEMA imewahakikishia wanachama wake kuwa, imejipanga vyema na ina uungwaji mkono mzuri katika majimbo mawili yanayofanya uchaguzi mdogo wa Wabunge ya Monduli na Ukonga na wanategemea kuibuka na ushindi. 

Wabunge wa CHADEMA waliojiuzulu ni Godwin  Mollel, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Siha Mkoani  Kilimanjaro, Mwita Mwikwabe Waitara aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Monduli Julius Kalanga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad