Kila Mfiwa Ajali ya MV Nyerere Kulipwa Milioni 1 Badala ya Laki 5

Kila Mfiwa Ajali ya MV Nyerere Kulipwa Milioni 1 Badala ya Laki 5
Rais John Magufuli ameagiza wafiwa wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kupata Sh 1 milioni baada ya awali kupewa Sh 500,000 kila mmoja.

Hata hivyo watu 41 walionusurika kwenye ajali hiyo nao watapewa Sh1 milioni kila mmoja.

Fedha hizo zinatokana na michango ya kampuni, watu na taasisi mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuchangia waathirika hao.

Awali, familia za waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo iliyotokea Alhamisi iliyopita walipewa Sh500,000 kwa kila mtu aliyefariki, fedha ambazo zimepatikana kutokana na michango ya Watanzania, kampuni na taasisi mbalimbali.

Akizungumza na vyombo vya habari jana kisiwani Ukara wilayani Ukerewe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe alisema leo wataanza kutoa fedha hizo kama walivyoagizwa na Rais Magufuli kwa familia za marehemu na wote walionusurika.

“Rais ameniagiza niwaambie kwamba fedha kwa waliopoteza ndugu zao na wale 41 walionusurika, sasa watapata Sh1 milioni kila mmoja. Kuanzia kesho (leo) tutaanza kutoa fedha hizo, wapeni taarifa,” alisema Kamwelwe.

Alisema kiwango cha fedha kilichokusanywa mpaka jana jioni ni Sh397 milioni ambazo zimetolewa na watu na taasisi mbalimbali. Alisema Rais Magufuli amesema fedha hizo ni za wananchi walioathirika na ajali hiyo.

Waziri huyo alisema mpaka kufikia jana jioni, miili miwili ya watoto ilipatikana wakati kazi ya kukiinua kivuko hicho ikiendelea na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kufikia 226.

Kuhusu kurudisha hali ya usafiri katika kisiwa hicho, Kamwelwe alisema leo au kesho kitapelekwa kivuko kingine kinachoitwa Mv Temesa ambacho kiko Mwanza kwa ajili ya kutoa huduma wakati shughuli ya kukiinua kivuko cha Mv Nyerere ikiendelea.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad