KUNA picha ambalo mashabiki wa Yanga walikuwa wanakuna vichwa kwa vile walikuwa hawaelewi linaendaje. Lile la Kiungo wao Mzanzibar, Mohammed Issa ‘Banka’ waliyemsajili kwa gharama kutoka Mtibwa.
Ukweli ni kwamba Banka amesimamishwa au kufungiwa kucheza soka kwa miezi mitatu.
Adhabu hiyo imetolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambalo lilibaini Banka kutumia madawa yanayoongeza nguvu ambayo hayakubaliki michezoni.
Kutokana na hali hiyo, Fifa imeamua Banka kutocheza kwa miezi mitatu na atakuwa chini ya uangalizi wake. Baada ya hapo, wataalamu wake watatua nchini kuchukua vipimo tena ili kupata uhakika kama anatumia au la.
Habari za uhakika kutoka jijini Zurich zimeeleza, Banka amefungiwa baada ya kubainika alitumia kilevi hicho kwa zaidi ya asilimia 150.
“Alitumia kilevi hicho kwa zaidi ya asilimia 150, nafikiri ilifika 200 na kitu. Lakini Fifa wanamuona bado mdogo, wametoa nafasi ya miezi mitatu. Maana wakati wa kumhoji alitoa ushirikiano kwa asilimia kubwa sana, wakaona wampe nafasi ya kujirekebisha,” kilieleza chanzo cha uhakika.
“Viongozi wa soka hapo wamekuwa wakificha, lakini TFF wanajua muda mrefu. Huenda walifanya hivyo kulinda maadili kutokana na kazi yao. Yanga pia wanajua, wamekuwa wakificha tu,” kilisisitiza chanzo.
Banka alipimwa wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji, Kenya wakati Zanzibar ilipotinga fainali ya michuano hiyo na kufungwa na wenyeji.
Taarifa nyingine zinasema baada ya Banka kung’ara wakati Taifa Stars ikiitwanga DR Congo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ndipo wataalamu hao wa Fifa walipojiridhisha kuhusiana naye na kubaini kweli alikuwa akitumia kilevi hicho.
Kwa mujibu wa sheria za Fifa, anayebainika anatumia madawa kwa kiwango zaidi ya asilimia 150, hufungiwa hadi miaka minne lakini chanzo kingine kutoka jijini Nairobi ambako yalichukuliwa majibu hayo kimesema:
“Kwa huyo kijana wenu akifungiwa labda miaka miwili. Fifa waliona amewapa ushirikiano lakini wanamchukulia kama kijana anayekua. Lakini wakiona ameacha kabisa, basi atasalimika.”
Yanga walimng’oa mchezaji huyo mikononi mwa Simba na Singida United ambazo nazo zilikuwa zikimmezea mate, lakini Championi Jumatano hatimaye limebaini ukweli baada ya kufanya uc hunguzi wa kina ndani ya Yanga pamoja na kwa maswahiba wake wa karibu mjini Unguja.
Banka amekuwa haonekani Yanga tangu asajiliwe msimu huu, huku baadhi wakihisi kwamba aliingia mitini kutokana na kutomaliziwa mkwanja wake.
Lakini yeye mwenyewe licha ya kuitwa mara kadhaa kwenye mazoezi ya Yanga hajatokea, amekuwa akiwaambia waandishi kwamba anaumwa na anajitibia mwenyewe kwao. Jambo ambalo timu yetu ya waandishi ilifanya uchunguzi na kubaini kwamba jamaa kapigwa pini na Fifa kwa muda wa miezi mitatu.