Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea amemgeukia Mwita Waitara aliyetimkia CCM kutoka katika chama hicho kikuu cha upinzania, akimtaka aache kufuatilia mambo yake.
Kubenea ambaye hivi karibuni alikuwa kwenye mijadala baada ya barua iliyoaminika kuwa ni ya kwake ya kuomba kujiuzulu kusambaa mitandaoni, amemtaka Waitara ‘kuachana naye’ huku akikanusha pia taarifa ambazo mbunge huyo wa zamani wa Ukonga alizitoa kwenye mikutano ya kampeni.
Waitara, akiwa kwenye mkutano wa kampeni akiwaomba tena wananchi wa Ukonga kumpa nafasi ya kuwa mbunge wao kupitia CCM, alisema kuwa Kubenea anaweza kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge kutokana na shida iliyo ndani ya Chadema.
“Jimbo la Ubungo litaweza kuwa wazi wakati wowote kuanzia sasa. Kuna shida ya uendeshaji ndani ya Chadema,” Waitara alikaririwa.
Akijibu kauli hiyo, kwanza kubenea alikanusha kuandika barua ya kujiuzulu akiikana barua iliyosambaa mitandaoni kabla hajamkana Waitara pia.
“Hiyo barua mimi naiona mitandaoni, sio barua yangu na wala siijui,” Kubenea anakaririwa na Mwananchi. “Witara afanye mambo yake, asitumie kivuli changu na aache kunifuatafuata,”ameongeza.
Vuguvugu la tetesi za kuwa huenda Kubenea akawa mbioni kuachana na Chadema zilianzia mitandaoni, watu wakiyapitia maandishi yake na kuyatafsiri kwa mlengo huo. Lakini pia, barua mbili zilizosambaa mitandaoni, moja ikionekana kuwa ni yake na nyingine ya uongozi wa Chadema ukimpa onyo na kutaka ajieleze.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Vicent Mashinji pia alikana kuzitambua barua hizo na kudai kuwa yeye pia ameziona mtandaoni. Kubenea pia alikana kupokea barua yoyote ya kupewa onyo.