Kweli Dunia Imeisha! Askofu Aburuzwa Kortini kwa Tuhuma za Wizi wa Mahindi ya Yatima

Kweli Dunia Imeisha! Askofu Aburuzwa Kortini kwa Tuhuma za Wizi wa Mahindi ya Yatima
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imemfikisha Askofu wa kanisa la Gospel Ministry, Christopher Madole, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa kukabiliwa na mashtaka mawili, likiwamo la uchepushaji wa mahindi ya watoto yatima.

Katika shtaka lingine anakabiliwa na kosa la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu Mary Senapee, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Biswaro Biswaro, alisema kati ya Januari na Machi 2016, Askofu Madole, alichepusha mahindi tani 360 kutoka katika Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), aliyochukua kwa ajili ya kupeleka kwa familia maskini za Wilaya za Bahi na Chamwino na badala yake akayauza kwa mtu mwingine na hivyo kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Aidha, taarifa kutoka kwa Kamanda wa Takukuru, Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, ilisema taasisi hiyo wilayani Kondoa imewafikisha mahakamani askari wanyamapori watatu wa pori la akiba la Mkungunero kwa kosa la kuomba rushwa ya Shilingi milioni nne.

Washtakiwa hao Steer Waliya, David Kayila na Nginanu Olepesa, walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kondoa wakituhumiwa kukamata ng'ombe 88 walioingia kwenye hifadhi na kupokea rushwa kutoka kwa wamiliki wa mifugo hiyo ili waiachie.

Wilayani Mpwapwa, Takukuru imemfikisha katika mahakama ya wilaya hiyo Lazaro Masimami, ambaye ni Ofisa Ardhi Msaidizi wa halmashauri ya wilaya kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh. 300,000 kwa mwananchi mmoja, ili amsaidie kupata hati ya kiwanja chake.

Wakati huo huo, Takukuru hivi karibuni imeshinda kesi ilizokuwa inaendesha wilayani Kondoa na Mpwapwa kwa mshtakiwa Saidi Abdalah, kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. 500,000 baada ya kutiwa hatiani kwenye shtaka la ubadhirifu na ufujaji na pia alitakiwa kurejesha Sh. 2,859,050 alizofuja wakati akiwa katibu wa kamati ya maji wa Kijiji cha Mwaikisabe, wilayani humo.

Aidha, Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa imewatia hatiani na kuwahukumu kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini, walimu wawili wa Shule ya Msingi Idilo, Henry Kindole na Peter Joctan, waliokuwa wanakabiliwa na shtaka la ufujaji na ubadhirifu wa fedha za mradi wa ujenzi wa shule hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad