Lugola: Marufuku Watumishi wa Wizara Yangu Kunyanyaswa

Lugola: Marufuku Watumishi wa Wizara Yangu Kunyanyaswa
Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka viongozi na watumishi mbalimbali wa wizara yake wafanye kazi kwa kushirikiana na kuacha tabia ya kunyanyasana wakati wanatekeleza majukumu yao ya kikazi.

Lugola pia amesema kila mtumishi wa wizara yake ana umuhimu mkubwa kwa kufanikisha mafanikio ya wizara hiyo kwakuwa watumishi hao wanafanya kazi kwa kutegemeana.

Akizungumza na watumishi wa makao makuu wa wizara hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Veta, jijini Dodoma jana, Lugola alisema kikao hicho alikiitisha kwa lengo la kujuana na watumishi hao pamoja na kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi.

“Mambo muhimu ambayo yatatuletea mafanikio ndani ya wizara yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa kushirikiana na tukifanya hivyo hakika tutapendana na kuzidi kufanikiwa,” alisema Lugola.

Lugola aliongeza kuwa, hapendi kuona mtumishi yeyote ananyanyaswa kwa kutopewa haki zake au kucheleweshewa pasipo kuwa na sababu za msingi ikiwemo malipo mbalimbali ya watumishi wanayodai, na endapo yatatokea hayo watumishi hao wamletee kero zinazowakabili ofisini kwake na kwa kushirikiana na katibu mkuu wa wizara hiyo watazitatua.

“Utumishi wa umma naujua, na pia nimepitia manyanyaso kadhaa mpaka leo nimefikia hapa kutokana na historia yangu, kwanini tusipendane?, kwanini tunyanyasane?, kwanini tusishirikiane?, ni tabia mbaya na inatakiwa kulaaniwa kwa baadhi ya wakuu wa idara na vitengo pamoja na wengineo ambao wanatabia ya kunyanyasa watumishi waliochini yao,” alisema Lugola.

Mkutano huo ambao ni wa kwanza kwa Waziri Lugola, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali, Jacob Kingu pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ramadhan Kailima, kuzungumza na watumishi wa Wizara hiyo tangu walipoteuliwa miezi kadhaa iliyopita, walitaka kujuana zaidi na watumishi wa wizara hiyo pamoja na kujua changamoto zao zinazowakabili. Toggle screen reader support
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad