Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ametekeleza ahadi aliyoitoa kwa Rais Magufuli Jumatano ya Septemba 5, 2018, ya kwenda kusikiliza na kutatua kero ya ardhi ya bibi Nyasasi Masige mkazi wa wilaya ya Bunda aliyedai kuporwa eneo lake.
Lukuvi jana ameanza ziara mkoani Mara akiwa na lengo la kusikiliza kero zote zilizoelezwa na wananchi wakati wa ziara ya Rais Magufuli mkoani humo. Ziara yake imeanzia wilayani Bunda na kufika moja kwa moja hadi nyumbani kwa bibi Nyasasi Masige kusikiliza kero yake.
Waziri Lukuvi ameutatua mgogoro huo kwa kuzikutanisha pande zote mbili ambazo ni bibi Nyasasi Masige na mfanyabiashara mmoja ambaye jina lake halijatambulika mara moja anayedaiwa kujimilikisha eneo zaidi ya lile alilouziwa awali na bibi Nyasasi.
''Nimewasikiliza vizuri na kutokana na kwamba eneo hili halijapimwa, nimeagiza mamlaka kulipima na kisha kumpatia viwanja viwili bibi Nyasasi'', alisema Lukuvi.
Aidha Waziri ameitaka mamlaka ya ardhi wilayani Bunda kuhakikisha zoezi la kupima eneo hilo linafanyika ndani ya siku nne na bibi Nyasasi amilikishwe viwanja hivyo viwili bila kutozwa gharama yoyote ya malipo ya Hati ya viwanja.
Katika ziara ya Rais Magufuli, bibi Nyasasi alieza kuwa alikuwa anamiliki eneo kubwa ambalo alilazimika kuuza kipande kwaajili ya kupata pesa ya matibabu na baada ya kwenda mjini Musoma kwa matibabu mtu aliyemuuzia alijimilikisha na eneo lililobaki bila maelewano.
Lukuvi Atatua Mgogoro wa Bibi Aliyemwaga Machozi Mbele ya Rais Magufuli
0
September 18, 2018
Tags