Maamuzi Ya Mahakama Baada Ya Mchungaji Msigwa Kusema Hajapata Wakili

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa anayekabiliwa na kesi ya jinai namba 112 ya 2018 na wenzake wanane, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado hajapata wakili wa kumtetea mahakamani hapo.

Mchungaji Msigwa leo Septemba 27, mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde amedai hadi sasa bado hajapata wakili hivyo ameiomba Mahakama muda ili aweze kupata wakili wa kumtetea katika kesi hiyo.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo, wanatetewa na wakili Peter Kibatala ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman  Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara ambaye pia ni Mbunge wa kibamba John Mnyika.

Wengine ni mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, mbunge wa Kawe, Halima Mdee, mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Msigwa ameeleza hayo mara baada ya Wakili wa Serikali, Simon Wankyo kueleza kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali (PH) na kwamba Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayeisikiliza kesi hiyo yupo likizo.

Wankyo ameendelea kueleza kuna rufaa namba 215 ya mwaka huu Mahakama ya Rufaa iliyofunguliwa na washtakiwa na inatarajiwa kutolewa uamuzi wiki ijayo katika tarehe ambayo watajulishwa hivyo ameiomba mahakama kuipanga kesi hiyo Oktoba 8, 2018.

Amedai anapendekeza tarehe hiyo kwa kuwa Hakimu Mashauri atakuwa amesharejea na Mahakama ya Rufaa watakuwa wameshatoa uamuzi.

Wakili Kibatala baada ya kusikiliza hoja hizo ameiomba mahakama iwapatie muda wa kutosha Oktoba 25, 2018 ili pia na mshtakiwa Msigwa aweze kutafuta wakili wa kumtetea. Pia siku hiyo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali kwa Hakimu Mashauri.

Hakimu Kasonde amekubaliana na ombi la kuahirisha kesi hiyo na aliiahirisha hadi Oktoba 25, 2018 ili kumpa muda wa kutosha Msigwa kutafuta wakili wa kumtetea.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad