Mabeyo: Tuko hatua ya mwisho kuisimamisha Mv Nyerere
0
September 25, 2018
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amesema wako katika hatua ya mwisho ya kukisimamisha kivuko cha Mv Nyerere kilichozama Septemba 20,2018.
Akizungumza leo Septemba 25, 2018, Mabeyo amesema wanahakikisha kivuko hicho kinasimama katika hali yake ya kawaida baada ya kufanikiwa kukigeuza na kuwa ubavu.
"Pia tunaendelea na uokozi wa baadhi ya miili ambayo huenda ilikuwa imelaliwa na mizigo hadi pale tutakapojihakikishia kuwa tumeimaliza yote ndani ya kivuko hiki" amesema Mabeyo.
Awali, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe amesema michango iliyochangwa leo ni Sh160.3 milioni kutoka Taasisi za fedha, kidini na wavuvi.
Michango hiyo ni Benki ya KCB (125 milioni), Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam (Sh25 milioni), Benki ya Posta (Sh10 milioni) pamoja na wananchi John Salia (Sh100,000) na Abel Michael(200,000).
Waziri Kamwelwe amesema kupokelewa kwa michango hiyo kumefanya kiasi katika akaunti kufikia Sh557 milioni ambayo itatumika kuwalipa wafiwa na walionusurika katika ajali hiyo.
"Tunaomba muendelee kutuchangia kupitia akaunti yetu iliyo katika benki ya NMB na kupitia namba ya simu maalumu na muamini kuwa pesa hizo hazitatumika nje ya shughuli hii," amesema Kamwelwe.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mchango kwa niaba ya Benki ya KCB Tanzania,
Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Zuhura Muro amesema salamu hizo za pole zimetoka katika nchi za Afrika ya Mashariki kutokana na kuguswa na msiba huo.
"Msiba huu hauelezeki, ni mzito sana na unaonyesha jinsi gani maisha ya mwanadamu ni mepesi hivyo tunamuomba Mungu aendelee kuwapa nguvu wanaoendelea kufanya kazi ya uokoaji katika eneo hili," amesema Zuhura.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kama kanisa linaendelea kuratibu michango mbalimbali inayoweza kuwa msaada kwa waathirika hao.
“Mbali na kukabidhi mchango huo pia tuko nanyi katika sala ili kuhakikisha shughuli hili inaisha salama,” amesema .
Mvuvi John Salia kwa niaba ya mwenzake amesema wananchi wanapaswa kuchangia chochote walichonacho ili kuwasaidia waathirika hao.
Tags