Msanii wa muziki wa bongo fleva ambaye pia ni baba wa watoto wawili, Madee Ali amewashauri wanaume wenzake kufuta fikra walizokuwa nazo, kwamba mtoto anapaswa angaliwe na mama pekee na badala yake amewataka wawe karibu na watoto zao kwa lengo la kuwasaidia kufikia malengo yao.
Madee ameeleza hayo leo Septemba 21, 2018 alipokuwa anazungumza kwenye DADAZ inayorushwa na EATV, baada ya kuwepo dhana kwa baadhi ya wanaume kuwa mwanamke ndio mwenye wajibu wa kuangalia familia (malezi) pamoja na kujua watoto maendeleo yao.
"Moja ya ndoto zangu nilizokuwa nazo mimi ni kutaka kubadilisha fikra za ulimwengu hasa wakina baba ambao wamezoea kwa kusema wa mama pekee yake ndio anapaswa kumlea mtoto na kumuangalia kwa kila jambo. 'So' mimi nataka niwaambie vijana wenzangu tutoke huko, maana hakuna jambo zuri kama mwanamke kumuona mume wake akimsaidia katika malezi ya watoto. Tukae karibu na familia zetu pamoja na watoto ili kusudi tuweze kuwatambua mapema wanachohitaji katika kufikia kwenye ndoto zake hapo baadae", amesema Madee.
Mbali na hilo, Madee pia amewaonya wazazi wa kiume kuacha mazoea mabaya kwa mabinti zao ambao wamefikia katika umri wa kuvunja ungo, kwasababu wanapelekea jamii kuwafikilia vibaya pamoja na kuchafua taswira nzima ya wakina baba katika kusaidia familia zao.