Manusura FEKI waibuka mgawo wa milioni moja za Ajali MV Nyerere

Baada ya serikali kutangaza nyongeza ya Sh. milioni moja kwa kila ndugu aliyefiwa na ndugu yake katika ajali ya kivuko cha MV. Nyerere, wameanza kujitokeza watu wakidai na wao walikuwa kwenye kivuko hicho.

Hata hivyo, serikali imeushtukia utapeli huo na kuweka wazi kuwa hakuna mtu yeyote wa aina hiyo atakayepewa fedha hizo.

Akizungumzia suala la watu kujitokeza kudai fidia, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema hawatatoa fedha zozote kwa mtu ambaye hayumo katika orodha ya waliofariki na manusura.

Waziri Kamwelwe alisema kuwa idadi inayotambuliwa na serikali ni watu waliofariki ambao ni 228 na waliookolewa ni 41 tu.

“Yule anayejidanganya kujitokeza eti alikuwa katika kivuko ili alipwe huyo asahau, alikuwa wapi kujitokeza siku ile au kesho yake ambapo serikali ilikuwa hapa inafanya uhakiki,” alisema Waziri Kamwelwe jana na kuongeza:

“Idadi ikiongezeka ni ya wale marehemu watakaopatikana na tukajiridhisha ndugu waliojitokeza ni halali watapatiwa fedha zao na si vinginevyo.”

Aidha, Kamwelwe alisema idadi ya miili imefikia 228, ingawa kulikuwapo na taarifa ya kuonekana kwa miili miwili katika kijiji jirani.

Hata hivyo, alieleza kuwa ulikutwa mwili mmoja, hivyo idadi kufikia 229 si sahihi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad