Mazishi ya Waliopoteza Maisha Kwenye MV. Nyerere Kufanyika Kitaifa

Mazishi ya waliopoteza maisha kwenye MV.Nyerere kufanyika Kitaifa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema mazishi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya Mv.Nyerere iliyotokea Septamba 20 huko kisiwani Ukara, Ukerewe mkoani Mwanza yatakuwa ya kitaifa ambapo viongozi wakuu wa kitaifa wanatarajia kushiriki mazishi hayo.

Mhandisi Kamwelwe amesema shughuli za mazishi hayo zitagharamiwa na Serikali na kwamba utaratibu kamili wa eneo yatakapofanyika mazishi hayo utatolewa baadaye.

Hata hivyo Mpaka sasa zoezi la uokoaji na uopoaji wa miili ya watu waliokuwa kwenye kivuko cha MV.Nyerere linaendelea ambapo miili 100 ya watu imeopolewa na waliookolewa wakiwa hai wanazidi 40.

Vikosi vya uokoaji mkoa wa Mwanza vimeongezewa nguvu na vikosi vya mkoa wa Mara katika eneo la tukio ili kuongeza kasi ya kuopoa miili ya watu waliopinduka na kivuko hicho.

Aidha uongozi wa wakala wa meli mkoa wa Mwanza umetambua wafanyakazi wa kivuko watano ambao wamepoteza maisha akiwemo   nahodha, fundi, Karani, mlinzi na mkuu wa kivuko, Kivuko hicho kilikuwa na wafanyakazi wanane.

Mamia ya wakazi wa Ukerewe wamekusanyika nje ya kituo cha afya cha Bwisya kutambua miili iliyoopolewa kwenye ajali ya kivuko cha MV.Nyerere iliyotokea wakati wakisafiri kutoka kisiwa cha Bugorora kwenda Ukara kwenye gulio.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad