Mbunge wa Serengeti (Chadema) Chacha Marwa amesema Tume ya Uchaguzi (NEC) haiwezi kuwa huru kwa kuwa wakurugenzi ambao kimsingi ndio wasimamizi wa uchaguzi, waligombea ubunge na kushindwa, hawajawahi kujiuzulu uanachama katika vyama vyao.
Ametoa kauli hiyo jana Jumanne Septemba 4, 2018 wakati akiuliza swali ya nyongeza bungeni.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ofisa wa NEC hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
“Lakini wakurugenzi wengi ni wanachama wa CCM, wengi waligombea ubunge. Walioshindwa wameteuliwa lakini hawajajiuzulu ubunge. Matokeo yake wananyimwa fomu ama wanajificha wakati wa kurudisha fomu, “ alisema.
Alisema walinzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) maarufu green guard wamekuwa wakiwateka wapinzani wakati wa mikutano ya kampeni, hata yeye amewahi kukumbwa na jambo hilo.
“Hivi ndio tume huru ya uchaguzi? Huku tunapoenda mnataka hadi damu imwagike?” Alihoji Marwa na kukatizwa na Spika wa Bunge Job Ndugai.
Ndugai alimueleza mbunge huyo kuwa maswali yake mawili yanatosha, anakoelekea anaweza kuzungumza kauli za kichochezi.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde alisema NEC inapimwa kutokana na majukumu yake kikatiba yalivyoainishwa katika ibara ya 74 ya Katiba.
“Ibara ya 74 ya Katiba imeainisha majukumu ya tume yakiingiliwa ndio tume inakosa uhuru. Sitaki kuamini kuwa tume sio huru,”alisema.
Kuhusu kutekwa, Mavunde alisema suala la kutekwa si la NEC bali ni kosa la kijinai na kwamba anatakiwa kuripoti polisi