Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Nicholuas Matiko ameanika maisha yake nje kazi ya ubunge, ikiwemo matumizi na matunzo ya nywele zake.
Mbunge huyo machachari pindi awasilishapo hoja zake ndani na nje ya bunge, aliweka wazi maisha yake hayo, hivi karibuni katika mahojiano na Amani baada ya kumnasa ‘akiweka sawa’ nywele zake kwenye saluni moja iliyopo maeneo ya Kinondoni jijini Dar.
Matiko alisema, gharama za kutunza nywele zake hutegemea staili, lakini mara kadhaa humgharimu zaidi ya shilingi 80, 000 hadi 130,000 licha ya kudai anaishi maisha ya kawaida!
“Inaanzia hapo (80,000), wakati mwingine huwa inaongezeka lakini kiwango cha juu kabisa ni laki moja na thelathini na hii huwa inatokea pale ninapokuwa na mwaliko fulani mkubwa,” alisema Matiko. Hata hivyo, Matiko alisema wakati mwingine humchukua mwezi mzima bila kwenda saluni kutokana na ufinyu wa muda, lakini kwa kawaida huenda kila wiki.
“Shughuli za kibunge, kuwatumikia wananchi wa Tarime na mambo ya familia wakati mwingine yanabana kidogo unaweza kujikuta wiki imepita hujaenda kabisa saluni.” Matiko amewahi kuwa mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kati ya mwaka 2006 hadi 2016.
Pia, kuanzia mwaka 2010 amekuwa mbunge wa viti maalum (Chadema) kisha baadaye kuchaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, mwaka 2015 hadi sasa.