Mhandisi wa kivuko cha Mv Nyerere, Agostino Charahani aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza yupo chini ya ulinzi, MCL Digital imeelezwa leo Alhamisi Septemba 27, 2018.
Mmoja kati ya madaktari wanaomhudumia mhandisi huyo kwa sharti la kutotajwa jina ameieleza MCL Digital kuwa mhandisi huyo analindwa.
Charahani aliokolewa akiwa hai, ikiwa ni baada ya kupita saa 48 tangu kivuko hicho kupinduka Machi 20, 2018.
"Hapa watu hawajui kwamba maofisa wa usalama wapo wanazunguka humu. Inakuwa vigumu kuwabaini maana wamevalia kiraia," amesema daktari huyo.
Habari zaidi zinaeleza kuwa mhandisi huyo anashikiliwa kutokana na sababu kubwa mbili ambazo ni kumuepusha na wananchi wenye uchungu wa kupoteza ndugu katika ajali hiyo na kutoa ushahidi jinsi kivuko kilivyopinduka.
"Hapa huwezi kutoa hukumu ya moja kwa moja kuhusiana na mhandisi huyo kupewa ulinzi wanaomshikilia wanajua na wana sababu zao,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo, ofisa habari na mahusiano wa Bugando, Lucy Mogele alipoulizwa kuhusu mhandisi huyo alikataa kuzungumza.
Kivuko cha Mv Nyerere kimenyanyuliwa leo ikiwa ni siku ya saba tangu kilipopinduka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 228.