Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Injinia Isaac Kamwelwe amesema michango ya kusaidia waathirika wa ajali ya Mv Nyerere ambayo ilipelekea vifo vya mamia ya watu katika kisiwa cha Ukara imeshafikia milioni 557 huku zoezi la ugawaji wa fidia kwa familia hizo likiwa limekwisha anza.
Akizungumza wakati akipokea misaada kutoka kwa taasisi mbalimbali leo ikiwemo Kanisa katoliki jimbo kuu la Dar es salaam Waziri Kamwele amesema kwa leo kamati hiyo imepokea shilingi milioni 160.
“Kwa leo kuanzia asubuhi mpaka sasa hivi akaunti yetu ya maafa imepokea milioni 160 na jumla ina shilingi milioni 557, tumeshanza kulipa wafiwa kila aliyepoteza maisha ndugu yake atapatiwa shilingi milioni 1 kuanzia leo, na fedha tunayotumia ni hii ambayo watanzania wamewachangia wenzao ndo tunayoigawa..” Amesema Waziri Kamwelwe.
Akizungumzia zoezi la utoaji wa kivuko cha Mv Nyerere kilichozama Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Venance Mabeyo amesema wamefikia hatua za mwisho za kuhakikisha kivuko hicho kinasimama kama kawaida.
“Tumejitahidi kukinyanyua lakini kililala ubavu, Mafundi wanaendelea kufunga vifaa vya kusaidia kukiokoa, vilevile tunaendelea na uokozi wa miili na asubuhi hii tumepata maiti moja, tutahakikisha tunaimaliza shughuli hii mapema.” Amesema Jenerali Mabeyo.