Baadhi ya wanadiplomasia nchini wamekuwa na mtazamo tofauti kuhusiana na ziara ya mke wa rais wa Marekani, Melania Trump, anayetarajia kuzuru bara la Afrika, Oktoba mosi, akiambatana na ujumbe ndani ya serikali ya Marekani.
Katika mahojiano na www.eatv.tv Mwanadiplomasia na Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia nchini Dkt. Bernard Achiula, amesema ni kitu cha ajabu na dharau kuona Rais Trump anamtumia mke wake kama nyenzo ya kusafisha hali ya kisiasa iliyopo baina ya Rais huyo na bara la Afrika.
“_Ni kitu cha ajabu kuona anamtuma mke wake, ni jambo la kutudharau na sio la kushabikia,dunia nzima inamjua Trump kwa kauli zake na kwa sasa yupo katika kusafisha siasa zake barani afrika,anafikiri kutuletea mke wake afrika tutampokea kwa sababu ni mwanamke, hili si jambo la maaana kabisa.”_ Amesema Dr. Achiula.
Melania Trump anatarajia kuzuru nchi nne ambazo ni Ghana,Misri,Malawi na Kenya kwa upande wa Afrika ya Mashariki ambao kwa sasa nchi ya Kenya imekuwa mshirika mzuri wa Marekani ,kuhusiana na hilo Dr achiula anasema,
“_Nchi ya Kenya imekuwa ni ya kuwasapoti Makaburu tangu wakati wa kupigania uhuru, sio watu wa kuwaamini katika siasa za Afrika na wala si nchi nzuri ya kuiga kama mfano kutokana na siasa yao,ukabila, mauaji na mengineyo kwahiyo ziara ya Melania Trump ni muendelezo wa siasa za Kenya katika kujipendekeza kwa taifa hilo la Marekani.”_
Ziara hiyo ambayo imeleta sura mpya katika medani za kimataifa ,inalenga kuisaidia Afrika katika masuala ya elimu,kupambana na ujangili wa wanyama pori, huduma bora kwa mama na mtoto pamoja na kujikinga na Virusi vya Ukimwi.
Mpaka sasa Donald Trump hajazuru katika bara la Afrika tangu aingie madarakani na ameshutumiwa kwa kutoa maneno ya kejeli na matusi mapema mwaka huu, yaliyoelekezwa kwa nchi za Afrika.