Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu Musukuma (CCM), amesema viongozi wengi wa vyama vya upinzani wanataka kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Musukuma ameyasema hayo jana kwenye uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani Kata Machame Uroki wilayani Hai, uliofanyika katika Viwanja vya Kurasinde ambapo pia amesema ifikapo Septemba 10 mwaka huu, nguzo za umeme italetwa katika kata hiyo ili wananchi waondokane na tatizo la umeme huku akiwataka kumchagua mgombea udiwani wa jimbo hilo kupitia CCM, Robson Kimaro.
“Viongozi wengi wanaitaka CCM, sasa nawasihi wananchi mliopo katika vyama vya upinzani kujitafakari kama mko sehemu salama,” amesema.
Aidha, akizungumzia kuhusu umeme katika wilaya hiyo amesema: “Sisi tutakwenda kumwagiza waziri mwenye dhamana na sasa tunapozungumza Meneja wa Tanesco (Shirika la Umeme nchini), Mkoa wa Kilimanjaro amesema nguzo zipo tayari kwa hiyo ndani ya siku 10 tatizo lenu la umeme litakuwa limekwisha katika vijiji hivyo viwili vya Kurasinde na Bwera, ninachokizungumza nina uhakika nacho kwa sababu nipo ndani ya chama chenye serikali na kama nazungumza uongo nifukuzwe bungeni.”
Naye Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Sixtus Mapunda amesema, Robson alikuwa Diwani mzuri na mwenye nia ya kuwatumikia wananchi lakini tatizo alikuwa katika chama kisichojali maendeleo ya wananchi.
“Wananchi wa Machame Uroki mnahitaji maendeleo na si maneno, Robson baada ya kutambua hilo na kutambua dhamira yake ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo alitambua hawezi kutimiza lengo hilo ndani ya Chadema na kuamua kujiunga ndani ya CCM ili kuwaletea maendeleo hivyo naombeni mumuunge mkono kwa kumpa kura za kishindo,” amesema Mapunda.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi alisema kuwa, katika maneno ya mkoa huo ambayo wananchi wamewachagua viongozi wa vyama vya upinzani maendeleo yake yamekuwa yakirudi nyuma na kuwataka wananchi kutorudia makosa.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani Robson Kimaro amesema, kata hiyo ina changamoto ya uchakavu wa majengo ya Shule ya Msingi Mkwasaringe hali ambayo ni hatarishi kutokana na nyufa katika kuta hali ambayo imesababisha wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la nne kutumia darasa moja kusoma kwa kupokezana ambapo ameahidi kutaitatua changamoto hiyo.