Mtoto wa aliyekuwa mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi bongo, marehemu Ramadhan Masanja 'Banza Stone', Hans Stone amesema sababu kubwa ya yeye kujihusisha na masuala ya muziki ni kutaka kumuenzi baba yake kwa kile alichokuwa anakifanya enzi za uhai wake.
Hans Stone ameeleza hayo alipokuwa anazungumza na eNewz inayorushwa na tinga namba moja kwa vijana EATV, na kusema ameamua kuchagua kazi hiyo kutokana na kipaji alichokuwa nacho pamoja na kutaka kufanya yale yaliyoachwa na marehemu baba yake Banza Stone.
"Kupitia muziki huu ninaoufanya namuenzi baba yangu Banza Stone kwasababu na yeye alikuwa mwanamuziki, tupo njia moja ila kwa bahati nzuri yeye hayupo mimi nipo naendelea na nimevaa viatu vyake", amesema Hans Stone.
Mbali na hilo, Hans Stone ameithibitishia eNewz kuwa yeye ndio mtoto pekee aliyeachwa na marehemu baba yake na hakuna mtoto mwingine sehemu yoyote ile.
"Mimi ni mtoto wa kwanza upande wa baba kama baba ila mama ndio ana mtoto mwingine. Banza Stone ni alikuwa ni baba bora kwangu pia alikuwa ananipa moyo kabla ya kufariki kwake kwamba nipambane", amesisitiza Hans Stone.
Marehemu Banza Stone aliwahi kutamba akiwa na bendi mbalimbali zikiwemo Twanga Pepeta na TOT Band, na kufariki dunia Juli 17, 2015 katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Banza Stone katika enzi za uhai wake amewahi kutamba na nyimbo kadhaa zikiwemo, mtaji wa maskini, kumekucha, elimu ya mjinga, angurumapo Simba mcheza nani na falsafa ya maisha. Amewahi pia kuimba vibao kadhaa vya taarabu ukiwemo kuzaliwa mjini na ule wa Play Boy.