Mkurugenzi wa uchaguzi tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt. Athuman Kihamia amesema kuwa tayari imetuma jopo la watendaji ili kusimamia kazi za uhakiki na kusimamia shughuli zote zinazotakiwa kuendeshwa na tume ili kuondoa dosari zinajitokeza nyakati za uchaguzi.
Dkt. Kihamia amesema hayo kupitia East Africa BreakFast ya East Africa Radio, ambapo amefunguka kuwa tume imewapa vitazamio waangalizi hao wa uchaguzi ili kuhakikisha kila kinachotakiwa kufanyika kabla na baada ya uchaguzi kiko sawa.
“Kwa kipindi hiki hakuna mtendaji wa serikali bali anakuwa ni afisa wa tume ambaye amekula kiapo cha kuacha kazi zake zote za kichama na kila kitu zinakuwa pembeni na anakuwa chini ya sheria za tume”, amesema Dkt. Kihamia.
Dkt. Kihamia amesema kuwa waangalizi wa uchaguzi wanakuwa chini ya tume kwa siku 60 kwa mujibu wa sheria kwahiyo katika kipindi chote cha muda wa kampeni hadi kukamilisha zoezi la upigaji kura na kutangazwa kwa mshindi ndipo anaporejea katika majukumu yake ya kawaida na si kweli kwamba tume hutumia viongozi wa serikali bali ni wananchi kukosa uelewa juu ya hilo.
Uchaguzi mdogo wa marudio katika jimbo la Ukonga umekuwa na mvutano baina ya vyama vya CCM na Chadema kutokana na wagombea wake kuwa ndio wenye upinzani mkali mara baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema Mwita Waitara kujiuzulu na kurejea kugombea tena kwa tiketi ya CCM.