Baada ya kivuko cha Mv Nyerere kufikishwa nchi kavu leo, Rais John Magufuli ameagiza watu walioshiriki kwenye zoezi la kuokoa watu, kuopoa miili na kunasua kivuko hicho wapewe shilingi laki nne (400, 000) kila mmoja.
Hilo limethibitishwa na Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Isack Kamwelwe leo jioni, wakati akitoa shukrani kwa makundi mbalimbali yaliyoshiriki kufanikisha zoezi zima la kuokoa na kuopoa miili ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo iliyotokea Septemba 20.
''Rais anawashukuru sana kwa kazi hii, kuanzia mwanzo ameona jitihada zenu za kuokoa wenzetu na kwa kutambua mchango wenu ameagiza tuwapatie shilingi laki nne (400, 000) kila mmoja, kama sehemu ya pongezi zake'', amesema Kamwelwe.
Kamwelwe amethibitisha kuwa kivuko hicho kimefika nchi nchi kavu leo baada ya kukamilika kwa zoezi la kukinasua kutoka majini ambapo pia amesema kuna mizigo ambayo ilikuwa imebanwa kwenye kivuko na itaendelea kutolewa taratibu.
Ameongeza kuwa pamoja na shughuli hiyo kukamilika rasmi leo lakini baadhi ya vikosi vitaendelea na zoezi la kutafuta miili ambayo huenda imebaki kwenye maji na baada ya kujiridhisha watahitimisha kazi hiyo.
Ajali ya Mv Nyerere ilitokea Alhamis mchana, Septemba 12, ambapo zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha. Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba watu 100 na tani 25 kilikuwa kinafanya safari zake kati ya Kijiji cha Bugorora na kisiwa cha Ukara.