“Nitakuja kufukuza mwenyewe”- Magufuli

“Nitakuja kufukuza mwenyewe”- Magufuli
Rais Dkt. John Magufuli amesema kuwa hatosita kuwafukuza kazi watendaji wa Wizara ya Ujenzi pamoja na wakandarasi waliopewa tenda ya kujenga daraja la mto Sibiti endapo watashindwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na katika ubora unaohitajika.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa mradi wa daraja la Sibiti anauweka namba moja kwa kuufuatilia nakuahidi kuwa atakuwa akiwapigia simu wasimamizi mwenyewe na hatokuwa na muda wa kubembeleza mtu ili kukamilisha mradi huo kwa ufanisi.

Rais ametoa kauli hiyo leo Septemba 10, alipokuwa akikamilisha  ziara yake Mkoani Simiyu ambapo ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa daraja la Mto Sibiti linalounganisha mikoa ya Simiyu na Singida kupitia wilaya za Meatu na Mkalama ambapo amesema kuwa mkandarasi huyo anatakiwa kufanya kazi usiku na mchana bila kujali mvua wala kikwazo chochote na endapo ikitokea hivyo atafute njia mbadala.

“Hizi sababu walizotoa mawaziri na wahandisi za mkandarasi kuwa anajenga miezi minne sijui muda mwingine kuna mvua mimi nazikataa nataka hili daraja la Sibiti likamilike, ajenge usiku na mchana itakuwa miezi nane”, amesema Dkt. Magufuli

Ameongeza kuwa, “Mkandarasi ameshalipwa bilioni 18 za ujenzi anazo mfukoni, kwahiyo nawaomba wahandisi hili daraja likamilike mwezi wa tatu mwakani msitafute visingizio na inawezekana hata hii mitambo imeletwa haraka haraka jana walipojua nakuja, ndugu zangu wa wizarani naomba tuelewane kama mvua itanyesha mkandarasi atafute mbinu za kuzuia ili daraja likamilike ”.

Rais Magufuli amemaliza ziara yake leo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo alianza Septemba 3, jijini Mwanza ambapo amezindua miradi kadhaa ikiwemo utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa meli mpya na chelezo katika ziwa Victoria.

Baada ya kumaliza ziara katika mikoa hiyo Rais Magufuli anatarajia kufanya ziara katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe na Mbeya katika tarehe zitakazopangwa kwa mujibu taarifa iliyotolewa Agosti 30, na Gerson Msigwa ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad