ASKARI wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), John Soko (25), anatafutwa na polisi kutokana na kusababisha mauaji ya watu watatu baada ya gari lake kupinduka.
Soko ambaye ni askari katika kikosi kimoja mjini Arusha, ambaye yuko likizo, alipinduka na gari aina ya Toyota Brevis lenye namba za usajili T920 DGH alilokuwa akiendesha na kusababisha vifo hivyo katika tukio lililotokea juzi katika kijiji cha Ligunga, wilayani hapa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Jemen Mushy, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa baada ya tukio hilo, hiyo afisa huyo alikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda Mushy alisema katika tukio hilo, ofisa huyo alikuwa akitokea katika Hositali ya Misheni ya Kiuma kuchukua mwili wa marehemu Msusa Mtetechi baada ya kuombwa na wanafamilia hao.
Alisema akiwa njiani ofisa huyo aliendesha gari kwa mwendokasi hali ambayo ilimfanya ashindwe kulimudu baada ya kuyumba na kupinduka mara tatu na kusababisha vifo vya watu hao.
Kamanda Mushy aliwataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Issa Mtonyole (51), Fatuma Abeid (70) na kaka wa dereva huyo aliyetambulika kwa jina la Mbalale Hassan (31).
Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Mushy amewataka wananchi ambao wana taarifa zake alikokimbilia mtuhumiwa huyo, kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa askari huyo na kuwezesha sheria kuchukua mkondo wake.