Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Faidha Omary maarufu kama Sister Fey amekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa kosa la kukiuka maadili kwa kuchapisha maudhui yanayodhalilisha kwenye mitandao ya kijamii kwa amri ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv jioni ya leo na kusema kuwa aliiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kumfuatilia msanii huyo juu ya matumizi yake ya mitandao na mwishowe waliweza kumkamata Septemba 19, 2018 usiku na kumuweka kituo cha polisi mabatini ambapo kwa sasa anasubiriwa kupandishwa Mahakamani.
"Mchakato wa kumchukulia hatua Sister Fey umeanza muda mrefu na kimsingi mimi kama Naibu wa Waziri ambaye nipo katika wizara inayosimamia masuala ya sanaa likiwepo na suala zima la maadili kwasababu vitu ambavyo alikuwa anavifanya Fey kila mtanzania alikuwa anaviona na vitu ambavyo vipo kinyume na maadili ya kitanzania", amesema Shonza.
Aidha, Naibu Waziri Shonza amesema alitegemea kumuona Sister Fey kubadilika mwenendo wa tabia yake, pindi alipoitwa kwa mara ya kwanza na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) lakini ndio kwanza alizidisha kufanya vitendo viovu.
"Naomba tu, niwaambie wasanii kiujumla wafuate taratibu na misingi iliyowekwa kwani endapo watakiuka sisi tutaendelea kuwakamata na kuwaweka ndani ili kusudi sheria iweze kuchukua mkondo wake", amesisitiza Shonza.
Sister Fey ni miongoni mwa wanamuziki walioweza kujipatia umaarufu mkubwa mitandaoni kwa vituko vyake visivyokuwa na maadili licha ya jamii kumkanya lakini yeye hakuweza kuacha na kuendelea kufanya hivyo.