Kutokana na uwepo wa ajali mfululizo mkoani Mbeya, jeshi la polisi limeamua kuingilia kati na kusimamia mwenendo wa magari katika maeneo korofi hususani yenye miteremko mikali kama Iwambi, Mwansekwa na Igodima.
Akifafanua utaratibu huo mpya ambao wamejiwekea kwaajili ya kuhakikisha ajali za mara kwa mara zinaisha, kamanda wa usalama barabarani mkoani humo, Jumanne Mkwama, amesema wameamua kuwa wanayapitisha magari katika maeneo hayo kwa utaratibu maalum.
''Jeshi la polisi mkoa tumejadiliana na tumekubaliana kuwa tutasimamia na kupitisha magari ambapo utaratibu tuliouweka ni malori kuanza kisha magari ya abiria na magari madogo, ili kuepuka yasikutane kwenye mteremko na kusababisha ajali kama ambavyo imekuwa ikitokea'', amesema.
Kumekuwepo na mfululizo wa ajali katika mkoa wa Mbeya ambapo Mwezi Juni, watu 13 wakiwemo vijana 11 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), askari 1 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na dereva walipoteza maisha, kwenye mteremko wa Mwansekwa Mbeya.
Aprili, watu 8 waliokuwa kwenye gari ndogo aina ya Toyota Noah walifariki dunia papo hapo baada ya gari hilo kugongana uso kwa uso na basi katika eneo la Igodima. Na Septemba hii watu wapatao 15 walifariki dunia katika ajali iliyohusisha magari kwenye mlima Igawilo jijini Mbeya.
Hivyo katika kukabili ajali hizo kamanda huyo wa usalama barabarani amesema wameamua kusimamia kuyapitisha magari, kabla ya barabara hizo kupanuliwa ili magari yawe yanapishana vizuri yasigongane