Taarifa ya Kensington Palace inasema ingawa atakuwa katika ziara ya kibinafsi, ameombwa na Malkia kutekeleza shughuli kadha rasmi kwa niaba yake. Akiwa nchini Kenya, William atatembelea kikosi cha wanajeshi wa Uingereza cha 1st Battalion cha Irish Guards Battlegroup nchini Namibia, anatarajiwa pia kukutana na Makamu wa Rais, Nangolo Mbumba, na pia atahudhuria hafla ya kusherehekea ushirikiano kati ya Uingereza na Namibia katika makazi ya balozi wa Uingereza nchini humo Kate Airey.
William ameeleza wazi upendo wake kwa bara Afrika. Aliomba posa kutoka kwa mkewe Kate Middleton wakiwa katika mgahawa mmoja wa porini karibu na Mlima Kenya mwaka 2010. William, 36, majuzi alipokuwa anakubali kuwa mlezi wa shirika la Royal African Society alieleza anavyolipenda bara hilo.
“Nilianza kuipenda Afrika mara ya kwanza nilipokaa kwa muda Kenya, Botswana na Tanzania nikiwa bado kijana mdogo. Nilifurahia sana na nimekuwa nikitaka kurudi mara kwa mara kadiri iwezekanavyo tangu wakati huo,” alisema
Mara ya mwisho kwake kuzuru Kenya ilikuwa mwaka 2016 ambapo alikutana na Rais Uhuru Kenyatta na kushauriana kuhusu usalama na uhifadhi wa wanyama. Wengi watasubiri kuona iwapo atasafiri na Catherine ambaye amekuwa katika likizo ya uzazi tangu mwezi Machi alipojifungua mwanaye Louis.
Anatarajiwa kurejelea majukumu yake rasmi karibuni. Wamejaliwa watoto wengine wawili, George, 5, na Charlotte, 3. William ni wa pili katika orodha ya warithi wa kiti cha ufalme wa Uingereza baada ya babake Prince Charles.