Profesa Mwandosya Avunja Ukimya Sakata la Makontena Ya Makonda

Profesa Mwandosya Avunja Ukimya Sakata la Makontena Ya Makonda
Sakata  la makontena 20 yaliyoko Bandari ya Dar es Salaam kwa jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limemwibua waziri wa zamani katika Serikali ya awamu ya nne, Profesa Mark Mwandosya akikumbushia misingi ya utawala bora.

Makontena hayo yaliyokwama bandarini baada ya Makonda kushindwa kulipa kodi ya Sh bilioni 1.2, kwa mara ya pili juzi yalishindwa kuuzwa kwa mnada baada ya wanunuaji kushindwa kufikia bei.

Juzi, Profesa Mwandosya aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, akisema alivyofundishwa misingi ya utawala bora, mkuu wa nchi akimkosoa mtumishi hadharani, anapaswa kuandika barua ya kujiuzulu.

Ingawa hakumtaja Makonda moja moja, lakini ni wazi kuwa alimlenga mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuwa ni siku chache tu baada ya Rais Magufuli kumkosoa Makonda hadharani na kumtaka alipe kodi hiyo.

“Nilifundishwa misingi ya utawala, mkuu wa nchi akimkosoa mtumishi hadharani, unapeleka barua ya kujiuzulu ili kulinda heshima yake na kwa kufanya hivyo unajijengea heshima mbele ya umma. Nikiri kwamba huenda misingi hiyo imepitwa na wakati,”aliandika Profesa Mwandosya.

Jumapili ya Agosti 26 mwaka huu, Makonda alifanya ibada maalumu ya kumwomba Mungu ili wanaofanya mnada wasipate wateja.

“Amelaaniwa mtu yule atakayenunua furniture (samani) za walimu. Nimefanya ibada maalumu ya kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa sababu naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wanaofanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni jitihada zangu binafsi." Alisema Makonda

Kauli hiyo ya Makonda ilimwibua Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango siku moja baadaye, aliyeapa kusimamia sheria na kuhakikisha makontena hayo yanapigwa mnada

Alhamisi ya wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli aliingilia kati mzozo kuhusu makontena hayo ambao ulianza tangu Machi mwaka huu, akimtaka Makonda alipe kodi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad