Rais John Magufuli Atengua Kauli ya Waziri Kangi Lugola


Rais John Magufuli ametengua kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliyetaka wananchi wanaokutwa sokoni wakiuza samaki waliovuliwa kwa  njia haramu kutobughudhiwa.

Katika maelezo yake, Rais Magufuli ametaka wote watakaokutwa na samaki waliovuliwa kinyume cha sheria wawajibishwe kwa kutaja na kuonyesha walikopata samaki hao.

Leo Jumamosi Septemba 8, 2018, akisalimiana na wananchi katika mkutano wa hadhara mara baada ya Rais Magufuli kuweka jiwe la msingi wa mradi wa maji Lamadi, Lugola almetaka vita na operesheni dhidi ya zana na uvuvi haramu iwalenge wahusika wakuu ambao ni wavuvi.

Wengine aliotaka washughulikiwe ni wafanyabiashara na wamiliki wa zana haramu za uvuvi, si kuwasumbua akina mama wanaokutwa na samaki sokoni.

"Hawa wanaokutwa na samaki sokoni wasisumbuliwe kwa sababu hilo ni sawa na bao la mkono. Tushughulike na wahusika wakuu wa  zana na uvuvi haramu," amesema Lugola huku akitambuisha jina lake jipya la 'Nati ya daraja la Kirumi'.

Hata hivyo, akihutubia umma huo muda mfupi baada ya kauli hiyo ya Lugola, Rais Magufuli ameagiza wanaokutwa na samaki waliovuliwa kinyume cha sheria kuwajibishwa kwa  kutaja na kuonyesha walikopata samaki hao.

"Anayekutwa na samaki waliovuliwa kinyume cha sheria lazima waonyeshe walikowatoa. Tukishajua walikopatikana, mhusika pia atatuonyesha alikopata zana haramu," amesema Rais Magufuli.

"Hatuwezi kufanikiwa katika vita dhidi ya zana na uvuvi haramu kwa kuwategemea polisi na vyombo vya dola peke yao kwa sababu hatuna uwezo wa kuweka askari katika kila sehemu.  Kazi hii lazima ihusishe Watanzania wote na kila mtu pale alipo."

Ametumia mkutano huo kumuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kuagiza kukamatwa na kuswekwa mahabusu  kwa wenyeviti wa vijiji na mitaa ambao maeneo yao bado kuna zana na uvuvi haramu ili wasaidie uchunguzi kwa sababu ni lazima wanawafahamu wahusika.

Kwa mara nyingine, Rais Magufuli amemwagia sifa Mpina kwa kusimamia vyema operesheni dhidi ya zana na uvuvi haramu akimtaka kukaza uzi zaidi bila kujali kelele za watu wakiwemo wanasiasa.

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad