Hotuba za viongozi wa dunia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zimeingia siku yake ya pili mjini New York, Marekani ambako marais wa Afrika tayari wameshahutubia kikao hicho cha kila mwaka cha Umoja wa Mataifa.
Rais wa DR Congo Joseph Kabila ambaye alizungumza hapo jana alilihakikishia baraza hilo kuwa uchaguzi utafanyika nchini mwake mwaka huu, huku Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, akielezea umuhimu wa Waafrika kutatua mizozo ya Afrika wenyewe.
Rais Kabila amezikosoa vikali nchi zinazoingilia kati masuala ya ndani ya Congo na kusema ni kinyume na misingi ya kimataifa na kuhakikisha kwamba taratibu za uchaguzi nchini mwake haziwezi tena kupotoshwa. "Nimehakikisha kwamba uchaguzi uliotarajiwa Desemba mwaka huu utafanyika."
Rais huyo wa DRC aliendelea kusema "Hatuwezi kujenga Umoja wa Mataifa ikiwa kutakuwepo na moja wapo ya serikali inayoingilia kati masuala ya ndani ya nchi zingine. Ni mshangao kuona Umoja wa Mataifa umeendelea kuachia hali hiyo ikiendelea na kujipumbaza. Na ndio sababu msimamo wa nchi yangu ni ule wakukataa uingiliaji kati wa masuala ya ndani ya Congo." alisema Rais Kabila